Pata taarifa kuu

UN kutuma ujumbe wa haki za binadamu Karabakh wikendi hii

Umoja wa Mataifa utatuma ujumbe huko Nagorno-Karabakh wikendi hii ili kutathmini hasa mahitaji ya kibinadamu, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric ametangaza siku ya Ijumaa Septemba 28.

Raia watoroka Nagorno-Karabakh na kukimbilia Armenia kupitia eneo laa Lachin, Septemba 26, 2023.
Raia watoroka Nagorno-Karabakh na kukimbilia Armenia kupitia eneo laa Lachin, Septemba 26, 2023. AP - Vasily Krestyaninov
Matangazo ya kibiashara

Stéphane Dujarric amebainisha kwamba Umoja wa Mataifa  haujaweza kufikia eneo hili "kwa takriban miaka 30".

Takribani watu elfu 85,000 wameomba hifadhi nchini Armenia baada ya Azerbaijan kuudhibiti mkoa unaozozaniwa wa Nagorno-Karabakh huku shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, likisema idadi yao inaweza kuongezeka.

Msemaji wa serikali ya Armenia Nazeli Baghdasaryan, amesema hii leo kwamba idadi hiyo ya watu ni wale waliolazimishwa kukimbia makaazi yao katika mkoa wa Nagorno-Karabakh. Kwa mujibu wa taarifa ambazo hazijathibitishwa, Waarmenia wapatao 120,000 hapo awali, walikuwa wakiishi katika mkoa wa Nagorno-Karabakh. Mnamo wiki hii, Azerbaijan inayoongozwa na utawala wa kiimla, kupitia mashambulizi yake ya kijeshi ilichukua udhibiti kamili wa mkoa huo ambao umezozaniwa kwa miongo kadhaa.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR limethibitisha taarifa za kukimbia kwa idadi hiyo ya watu likitaja idadi kubwa zaidi ya elfu 88,000 na kwamba idadi yao inaweza kuongezeka kufikia 120,000.

Jamhuri isiyotambulika ya Artsakh ambayo ilikuwa ikiongoza jimbo la Nagorno-Karabakh ilitangaza wiki hii kuwa itahitimisha uwepo wake kuanzia Januari Mosi mwaka ujao. Waermenia waliokuwa wakiishi katika mkoa huo, wamekuwa na hofu ya kuteswa na vurugu kutoka upande wa Azerbaijan. Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan anaishutumu jirani yake Azerbaijan kwa kampeni ya "safisha safisha ya kikabila".

"Uhamaji wa Waarmenia kutoka Nagorno-Karabakh unaendelea kutokana na sera ya safisha safisha ya kikabila ya Azerbaijan. Uchambuzi unaonyesha kuwa katika siku zinazokuja hakutokuwa na raia hata mmoja wa Armenia atakayesalia Nagorno-Karabakh. Haya ni matokeo ya moja kwa moja ya kitendo cha safisha safisha ya kikabila na kuwaondoa watu katika nchi kama ambayo tumekuwa tukieleza jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu," amesema waziri mkuu Pashinyan.

Katika hatua nyingine wajumbe kutoka wizara za ulinzi za Azerbaijan na Armenia, wamewasili katika mji wa Urusi wa Tula kwa ajili ya mkutano wa baraza la mawaziri wa ulinzi wa nchi za Jumuiya ya Mataifa Huru CIS. Shirika la habari la Urusi, TASS limeripoti kwamba wajumbe kutoka nchi za Urusi, Azerbaijan, Armenia, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan watashiriki mkutano huo. Mkutano huo utajadili masuala kadhaa haswa juu ya ushirikiano wa kijeshi na hali ya sasa katika nyanja ya siasa za ulimwengu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.