Pata taarifa kuu

Hong Kong yatoa wito kwa wapinzani 8 walio uhamishoni kujisalimisha au kuishi 'kwa hofu'

Kiongozi wa Hong Kong John Lee Jumanne (tarehe 4 Julai) ametoa wito kwa wanaharakati wanane wanaounga mkono demokrasia wanaotuhumiwa kukiuka sheria za usalama wa taifa kujisalimisha. China pia "imetupilia mbali" ulinzi unaotolewa kwa baadhi yao na Uingereza.

Kiongozi wa Hong Kong John Lee.
Kiongozi wa Hong Kong John Lee. REUTERS - TYRONE SIU
Matangazo ya kibiashara

"Njia pekee ya kumaliza hatima yao kama wakimbizi, ambao watakuwa wakiwindwa maisha yao yote, ni kujisalimisha," John Lee amewaambia waandishi wa habari. Na kuongeza kwamba, vinginevyo, wanaharakati hawa wanane wataishi "kwa hofu".

Kundi linalolengwa linajumuisha waliokuwa wabunge wanaounga mkono demokrasia Nathan Law Kwun-chung, Ted Hui Chi-fung na Dennis Kwok Wing-hang. Pia ni pamoja na mwanaharakati wa zamani wa vyama vya wafanyakazi, Mung Siu-tat, na wanaharakati Elmer Yuen Gong-yi, Finn Lau Cho-dik, Anna Kwok Fung-yee na Kevin Yam Kin-fung.

Wanaharakati hawa wanane walitoroka baada ya Beijing kuanzisha sheria ya usalama wa kitaifa huko Hong Kong mwaka wa 2020 ili kukandamiza upinzani baada ya maandamano ya kuunga mkono demokrasia mwaka wa 2019. Wanatuhumiwa kushirikiana na vikosi vya kigeni kuhatarisha usalama, kitaifa, makosa ambayo yanaadhibiwa kwa kifungo cha maisha.

John Lee pia ametoa wito kwa watu kusaidia polisi, akiongeza kuwa hata "jamaa na marafiki" wa wanaharakati hawa wanaweza kutoa habari. Polisi wameahidi zawadi ya dola milioni moja za Hong Kong (euro 117,000) kwa habari kuhusiana na wanaharakati hawa.

Hatua iliyolaaniwa na Marekani, Uingereza na Australia, nchi ambapo baadhi ya wanaharakati wanaotafutwa wanaishi. "Siogopi shinikizo la kisiasa kwetu, kwa sababu tunafanya kile tunachofikiria ni sawa," kiongozi wa Hong Kong amesema Jumanne.

Miongoni mwa wanaolengwa ni Nathan Law, mmoja wa vigogo wa vuguvugu la kuunga mkono demokrasia, ambaye alitoroka Hong Kong na kuelekea Uingereza ambako alipata hifadhi ya kisiasa.

"Wanasiasa wa Uingereza wametoa ulinzi wao kwa wazi kwa wakimbizi hawa", amelaani katika taarifa kwa vyombo vya habari msemaji wa ubalozi wa China nchini Uingereza, akilaumu "kuingilia" kwa London katika masuala ya ndani ya China. Siku chache zilizopita ilisherehekewa kumbukumbu ya miaka 26 ya kurejea kwa koloni la zamani la Uingereza nchini China mnamo Julai 1, 1997.

'Kunyamanzisha upinzani'

"Hatutavumilia majaribio ya China ya kuwatisha na kuwanyamazisha watu binafsi nchini Uingereza na nje ya nchi," Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu. "Uingereza daima itasimamia haki ya wote ya uhuru wa kujieleza na kuwatetea wale ambao wanalengwa," aliongeza waziri huyo.

Marekani pia ilizungumza dhidi ya mfumo wa malipo ulioahidiwa na mamlaka ya Hong Kong. "Matumizi ya nje ya mipaka ya sheria ya usalama wa kitaifa iliyowekwa na Beijing inaweka mfano hatari ambao unatishia haki za binadamu na uhuru wa kimsingi wa raia ulimwenguni kote," msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alionya katika taarifa siku ya Jumatatu.

Tangu Beijing kuweka sheria ya usalama wa taifa, Uingereza na Marekani zimesitisha mkataba wao wa kurejeshwa watuhumiwa nchini humo na Hong Kong.

Nathan Law alitoa wito kwa wakaazi wa Hong Kong kutoshirikiana na polisi. "Mimi ni raia wa Hong Kong nikizungumza kwa niaba ya raia wenzangu wa Hong Konge," ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.