Pata taarifa kuu

Uchaguzi wa urais nchini Comoro: Upinzani waitisha maandamano siku ya Ijumaa

Upinzani nchini Comoro umetoa wito siku ya Alhamisi, Januari 18, wa maandamano siku ya Ijumaa, Januari 19, huku makabiliano yakisababisha mtu mmoja kupoteza maisha na takriban watano kujeruhiwa tangu kutangazwa kwa ushindi uliopingwa wa mkuu wa nchi anayemaliza muda wake Azali Assoumani, katika uchaguzi wa urais.

Moroni, mji mkuu wa Comoro
Moroni, mji mkuu wa Comoro TONY KARUMBA / AFP
Matangazo ya kibiashara

 

"Tunatoa wito kwa wakazi wote wa miji na vijiji vyetu kuifanya kesho Ijumaa kuwa siku ya kitaifa ya maandamano na kulaani uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu wa Azali na mamlaka yake," wamesema katika taarifa ya pamoja wagombea watano wa upinzani walioshiriki katika uchaguzi huu.

Siku ya Alhamisi, mivutano ya hapa na pale kati ya makundi ya vijana na vikosi vya usalama imeendelea huko Moroni. Katika vichochoro vya katikati ya jiji, makundi ya vijana, mara nyingi wakiwa wameficha nyuso zao, wamerusha mawe kuelekea upande wa polisi, ambao walijibu kwa mabomu ya machozi.

"Tumekuwa tukipambana kwa zaidi ya saa 24 kwa sababu hatukubaliani na matokeo ya uchaguzi. Ndiyo maana tulichoma majengo rasmi," ameeleza kijana mmoja aliyekuwa akiandamana akiliambia shirika la habari la AFP, ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Siku ya Jumatano, makabiliano yaliongezeka katika vitongoji kadhaa vya Moroni. Majengo yaliharibiwa na kuchomwa moto: nyumba moja ya waziri, majengo ya biashara ya serikali, ghala la mchele. Baadhi walivunja mabango ya uchaguzi ya rais aliyechaguliwa tena Azali. Vizuizi vya barabarani vilivyotengenezwa kwa marundo ya mawe na vipande vya mbao viliwekwa barabarani.

Watu kadhaa wamekamatwa lakini hakuna maelezo yaliyotolewa kwa umma. Maandamano ni nadra nchini yanayofanyika kwa mkono wa chuma, na upinzani wowote unazuiwa haraka.

Azali Assoumani alichaguliwa tena Jumapili katika duru ya kwanza kwa 62.97% ya kura lakini 16.30% tu ya ushiriki katika kura, kulingana na takwimu rasmi zilizotangazwa Jumanne jioni. Ushindi huu unapaswa kumruhusu kurejea kwa muhula wa tatu mfululizo na kusalia madarakani hadi mwaka 2029.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.