Pata taarifa kuu

Uchaguzi wa urais Comoro: Mtu mmoja afariki na watano kujeruhiwa katika makabiliano

Mtu mmoja ameuawa na watano kujeruhiwa nchini Comoro, katika makabiliano yaliyofuatia kutangazwa kwa ushindi, unaopingwa na upinzani, wa Azali Assoumani anayemaliza muda wake katika uchaguzi wa urais, huku mvutano ukiendelea Alhamisi katika mji mkuu.

Azali Assoumani amechaguliwa kwa muhula wa tatu mfululizo kama rais wa Comoro.
Azali Assoumani amechaguliwa kwa muhula wa tatu mfululizo kama rais wa Comoro. © AFP
Matangazo ya kibiashara

 

Mtu mwenye umri wa miaka 21 ameuawa, "huenda kwa kupigwa risasi", Dk Djabir Ibrahim, mkuu wa idara ya dharura katika hospitali ya Maarouf huko Moroni, ameliambia shirika la habari la AFP. Wengine watano walijeruhiwa", ameogeza.

Siku ya Alhamisi, mivutano ya hapa na pale kati ya makundi ya vijana na vikosi vya usalama imeendelea huko Moroni. Katika vichochoro vya katikati ya jiji, makundi ya vijana, mara nyingi wakiwa wameficha nyuso zao, wamerusha mawe kuelekea upande wa polisi, ambao walijibu kwa mabomu ya machozi.

"Tumekuwa tukipambana kwa zaidi ya saa 24 kwa sababu hatukubaliani na matokeo ya uchaguzi. Ndiyo maana tulichoma majengo rasmi," ameeleza kijana mmoja aliyekuwa akiandamana akiliambia shirika la habari la AFP, ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Siku ya Jumatano, makabiliano yaliongezeka katika vitongoji kadhaa vya Moroni. Majengo yaliharibiwa na kuchomwa moto: nyumba moja ya waziri, majengo ya biashara ya serikali, ghala la mchele. Baadhi walivunja mabango ya uchaguzi ya rais aliyechaguliwa tena Azali. Vizuizi vya barabarani vilivyotengenezwa kwa marundo ya mawe na vipande vya mbao viliwekwa barabarani.

Watu kadhaa wamekamatwa lakini hakuna maelezo yaliyotolewa kwa umma. Maandamano ni nadra nchini yanayofanyika kwa mkono wa chuma, na upinzani wowote unazuiwa haraka.

Azali Assoumani alichaguliwa tena Jumapili katika duru ya kwanza kwa 62.97% ya kura lakini 16.30% tu ya ushiriki katika kura, kulingana na takwimu rasmi zilizotangazwa Jumanne jioni. Ushindi huu unapaswa kumruhusu kurejea kwa muhula wa tatu mfululizo na kusalia madarakani hadi mwaka 2029. Upinzani ulishutumu "udanganyifu mkubwa" na "ujazaji wa kura", ukitaka kufutwa kwa uchaguzi.

Ikiwa na visiwa vitatu vya Grande Comore, Anjouan na Mohéli, Comoro ina wakazi 870,000, asilimia 45 kati yao wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kulingana na Benki ya Dunia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.