Pata taarifa kuu

UN imeonya  kuhusu uwezekano wa kusambaa kwa mzozo wa Sudan katika maeneo mengine

Umoja wa mataifa umeonya kuwa mzozo unaoendelea nchini Sudan, umeanza kusambaa katika maeneo mapya, hali inayotishia kutokea kwa mzozo wa kibinadamu.

Maelfu ya raia wa Sudan wametoroka mapigano yanayoendelea, wengi wakikimbilia nchi jirani ya Chad na Sudan Kusini
Maelfu ya raia wa Sudan wametoroka mapigano yanayoendelea, wengi wakikimbilia nchi jirani ya Chad na Sudan Kusini © Zohra Bensembra / Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mapigano ya miezi saba kati ya jeshi la serikali na wapiganaji wa RSF umesababisha vifo vya maelfu ya raia, watu wengine milioni saba wakiwa wamepoteza makazi yao.

Kwa mujibu wa UN, machafuko hayo yamechangia kuzuka kwa mapigano ya kikabila na ghasia zinazoelekezwa dhidi ya wanawake.

Msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa barani Afrika, mwanadiplomasia wa Ghana Martha Ama Akyaa Pobee, ameeleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kudorora kwa hali nchini humo.

Akizungumza katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Martha Ama Akyaa Pobee amesema Sudan inakabiliwa na hatari ya kutumbukia katika mzozo wa kibinadamu.

Makabiliano yalizuka nchini Sudan tarehe 15 ya mwezi Aprili kati ya jeshi chini ya uongozi wa Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Daglo.

Watu zaidi ya elfu tisa wameripotiwa kuawawa katika vita hivyo kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya kiraia na yale ya kufuatilia mizozo.

UN inasema mapigano hayo kwa sasa yamesambaa katika maeneo mapya kama vile Gezira, White Nile na majimbo yanayopatikana Magharibi mwa Kordofan, hali ambayo inawaweka raia zaidi katika hali ya hatari.

Pande hasimu nchini Sudan zilirejelea mazungumzo yanayolenga kupata suluhu ya kinachoendelea mwezi uliopita jijini Jeddah, mazungumzo yanayoongozwa na Marekani na Saudi Arabia.

Licha ya pande zote kuonyesha nia ya kupata suluhu ya kumaliza mapigano, makabiliano yameendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.