Pata taarifa kuu
USALAMA-SIASA

UN yapanga kutengeneza fursa ya 'kihistoria' kumaliza mgogoro nchini Libya

Raia wa Libya wanakabiliwa na "fursa ya kihistoria ya kushinda" mzozo ambao unaoikabili nchi yao tangu 2011, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema hivi punde siku ya Jumanne, huku akiwa na matumaini ya uchaguzi kufanyika mwaka huu.

Abdoulaye Bathily, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya na mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Tripoli, Machi 11, 2023.
Abdoulaye Bathily, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya na mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Tripoli, Machi 11, 2023. AFP - MAHMUD TURKIA
Matangazo ya kibiashara

"Nafasi ya kihistoria imefunguliwa kushinda muongo huu wa mgogoro," Abdoulaye Bathily, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika wiki za hivi karibuni, "kuna mabadiliko mapya nchini Libya. Mashauriano makubwa yanafanyika kati ya wadau wa usalama. Viongozi wa kitaasisi na kisiasa pia wanachukua hatua kusogeza mbele mchakato wa kisiasa," amebainisha.

Abdoulaye Bathily amekaribisha hasa kufanyika kwa mikutano kadhaa mwezi Machi na Aprili huko Tunis, Tripoli, Benghazi na Sebha ya wawakilishi wa kijeshi kutoka mikoa mbalimbali ya nchi ambao "walijitolea kuunga mkono hatua zote za uchaguzi, kukataa vurugu nchini Libya na kuchukua hatua za vitendo kwa ajili ya kuwarejesha salama watu waliokimbia makazi yao."

"Mikutano kati ya vitengo vya kijeshi na vikosi vya usalama kutoka Mashariki, Magharibi na Kusini ni mafanikio. Mikutano hii ina thamani kubwa ya kiishara kwenye njia ya kuelekea maridhiano na muungano wa nchi," amesema.

Lakini "mwelekeo huu mpya wa kitaifa" unapaswa kuwa "endelevu na kuimarishwa", amebainisha Bw. Bathily, akiongeza kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea na kazi yake ya upatanishi ili masharti yote ya "kisiasa, kisheria na usalama" yatimizwe ili uchaguzi uweze kufanyika mwaka huu.

Uchaguzi wa urais na wa wabunge, uliopangwa kufanyika mwezi Desemba 2021, uliahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na tofauti zinazoendelea, hasa kwa misingi ya kisheria ya chaguzi hizo na kuwepo kwa wagombea wenye utata. Libya inapitia mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu kuzuka kwa uasi mwaka 2011 uliyomuangusha Muammar Gaddafi baada ya miaka 42 ya udikteta.

Serikali mbili zinagombania madaraka, moja ikiwa na makao yake mjini Tripoli (magharibi) na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, nyingine ikiungwa mkono na shujaa wa mashariki mwa Libya, Marshal Khalifa Haftar. Mwezi Februari Bw Bathily alitangaza mpango mpya kujaribu kuvunja mvutano huo na hivi majuzi alitumai kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa "katikati ya mwezi Juni" kuandaa uchaguzi kabla ya mwisho wa mwaka 2023.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.