Pata taarifa kuu
USALAMA-UGAIDI

Somalia: Sita waangamia katika shambulio la Al Shabab dhidi ya ofisi ya meya mjini Mogadishu

Nchini Somalia, raia wasiopungua sita waliuawa siku ya Jumapili Januari 22 katika shambulio la wanamgambo wa Kiislam wenye itikadi kali wa Al Shabab, wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipojilipua katika mji mkuu Mogadishu. Katika ufyatulianaji risasi uliofuata, washambuliaji wote sita pia waliuawa na polisi inasema hali imerejea kuwa ya kawaida. Hili ni shambulio la hivi punde zaidi katika mashambulizi mengi ambayo yametokea tangu mwanzoni mwa mwaka.

Gari la wagonjwa likiegeshwa nje ya ofisi ya meya mjini Mogadishu baada ya shambulio la kigaidi la Al-Shabab, Januari 22, 2023.
Gari la wagonjwa likiegeshwa nje ya ofisi ya meya mjini Mogadishu baada ya shambulio la kigaidi la Al-Shabab, Januari 22, 2023. © Feisal Omar / Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kulingana na msemaji wa polisi ya Somalia, shambulizi lililenga ofisi ya meya wa Mogadishu, na lilidumu saa nne. Mshambuliaji wa kujitoa mhanga alilipua mkanda wake uliokua na vilipuzi na kusababisha uharibifu wa majengo, kisha ufyatulianaji risasi ukafuata dakika chache baadaye.

"Washambuliaji wote sita waliuawa. Watano wakati wa makabiliano ya na vikosi vya usalama, na mmoja alijilipua, Sadik Dubishe amewaambia waandishi wa habari na shirika la habari la AFP. Raia sita pia waliuawa wakati wa shambulio hilo, na hali imerejea kuwa ya kawaida. Wafanyakazi wote katika afisi ya meya waliokolewa, kwa mujibu wa polisi.

Shambulio hilo limedaiwa na wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali wa Al Shabab.

Wiki hii iliyopita, kundi hili lenye mfungamano na Al-Qaeda limeongeza mashambulizi dhidi ya jeshi. Ni wakati serikali ya Somalia, kwa msaada wa mashambulizi ya anga ya Marekani na kikosi cha Umoja wa Afrika, imeanzisha "vita kamili" dhidi ya Al Shabab, ambao wanamiliki maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Siku ya Ijumaa Januari 20, wanajeshi saba waliuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi, shambulio lililotekelezwa na Al shabab huko Galcad, mji ulioko katikati mwa nchi hiyo uliochukuliwa hivi karibuni na vikosi vinavyounga mkono serikali. Kamandi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (Africom) ilisema Jumamosi Januari 21 katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba shambulio hili lilitekelezwa na wapiganaji zaidi ya mia moja wa Al Shabab, na limegharimu maisha ya "takriban thelathini" miongoni mwao.

Jumanne, Januari 17, Waislam wenye itikadi kali walitekeleza mashambulizi mengine dhidi ya kambi ya kijeshi huko Hawadley, yapata kilomita 60 kaskazini mwa Mogadishu, na kuua wanajeshi 11.

Siku moja kabla, jeshi la Somalia lilitangaza kuwa limeuchukua, bila mapigano yoyote, mji wa Harardhere, ulioko karibu kilomita 500 kaskazini mwa Mogadishu ambao ulikuwa unadhibitiwa tangu 2010 na Al Shabab. Serikali ilibaini kwamba kurejeshwa kwenye himlaya yake kwa jiji hili "la kimkakati" ni "ushindi wa kihistoria".

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.