Pata taarifa kuu

Togo: Rais amfukuza kazi waziri wa jeshi na mkuu wa majeshi

Rais wa Togo Faure Gnassingbé amemfuta kazi Waziri wa jeshi na kumteua mkuu mpya wa majeshi kama sehemu ya mabadiliko makubwa kwenye wadhifa wa mkuu wa jeshi, kwa mujibu wa maagizo kadhaa ya rais yaliyosomwa Alhamisi jioni kwenye televisheni ya taifa.

Rais wa Togo Faure Gnassingbé, Februari 17, 2020.
Rais wa Togo Faure Gnassingbé, Februari 17, 2020. PIUS UTOMI EKPEI / AFP
Matangazo ya kibiashara

Maagizo hayo hayaelezi sababu za mabadiliko haya makubwa, ambayo yanakuja wakati nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi inakabiliwa na tishio linaloongezeka kutoka kwa makundi ya wanajihadi.

Tangu mwezi Novemba 2021, Togo imekumbwa na mashambulizi yasiyopungua matano, yakiwemo mawili mabaya kaskazini mwa nchi hiyo, eneo linalokumbwa na uvamizi wa wapiganaji wa kijihadi waliopo upande wa pili wa mpaka wake, nchini Burkina Faso.

"Bi. Marguerite Essossimna Gnakadè ameondolewa majukumu yake kama Waziri wa Majeshi", kulingana na agizo la kwanza la rais, ambalo linabainisha tu kwamba "ameitwa kwenye majukumu mengine".

Wizara ya Majeshi sasa itahusishwa moja kwa moja na ofisi ya rais, chini ya amri ya Bw. Gnassingbé, kama ilivyokuwa kuanzia mwaka 2007 hadi 2020, linaongeza agizo la tatu. Kwa hiyo hakutakuwa na Waziri mpya wa Jeshi.

Kanali Tassousti Djato, Mkuu wa zamani wa jeshi la Anga, amepandishwa cheo na kuwa jenerali na "kuteuliwa Mkuu wa Majeshi ya Togo (FAT)", kulingana na agizo la nne la rais. Anachukua nafasi ya Jenerali Dadja Maganawé, aliyeteuliwa kwa wadhifa huu mnamo Desemba 6, 2020.

Mali, Burkina Faso na Niger zinapambana na waasi wa kijihadi, na mataifa jirani ya pwani kama vile Benin, Ghana, Togo na Côte d'Ivoire yamekuwa na wasiwasi kwa miaka kadhaa kuhusu kukithiri kwa ghasia katika ukanda huo.

Mwishoni mwa mwezi Novemba, marais wa Benin, Togo, Ghana, Côte d'Ivoire na Burkina Faso, pamoja na viongozi wa Niger na Mali, walikutana mjini Accra na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya, Uingereza na Ufaransa ili kuimarisha ushirikiano dhidi ya wanajihadi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.