Pata taarifa kuu

Somalia yaomba msaada baada ya mlipuko wa mabomu, Mogadishu

Rais wa Somalia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwasaidia waliojeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu yaliyoua watu 100 mjini Mogadishu siku ya Jumamosi, huku tingatinga zikiendelea Jumatatu kusafisha eneo la mlipuko huo kwa kuwatafuta wahanga.

Askari wa usalama na magari ya kubebea wagonjwa yameegeshwa karibu na majengo yaliyoharibiwa baada ya shambulio la bomu lililotegwa katika magari mawili lililolenga wizara ya elimu mjini Mogadishu mnamo Oktoba 29, 2022.
Askari wa usalama na magari ya kubebea wagonjwa yameegeshwa karibu na majengo yaliyoharibiwa baada ya shambulio la bomu lililotegwa katika magari mawili lililolenga wizara ya elimu mjini Mogadishu mnamo Oktoba 29, 2022. AFP - HASSAN ALI ELMI
Matangazo ya kibiashara

Waislam wenye itikadi kali wa Al-Shabab wamedai kuhusika na shambulio hilo, ambalo ni baya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mitano, wakisema wapiganaji wao walilenga Wizara ya Elimu. Shambulio hilo pia liliwajeruhi takriban watu 300. Mabomu mawili yalilipuka katika magari maili Jumamosi kwenye barabara yenye shughuli nyingi. Bomu la kwanza lililipuka, dakika moja baadaye bomu lingine likalipuka.

Somalia, nchi iliyoko katika Pembe ya Afrika, imetumbukia katika machafuko tangu kuanguka kwa utawala wa Siad Barre mwaka 1991.

"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, ndugu wa Somalia na ndugu wengine (...) kutuma madaktari Somalia kusaidia hospitali kuwatibu waliojeruhiwa," Rais Hassan Sheikh Mohamud alisema Jumapili, akisisitiza kwamba idadi ya waathiriwa inaweza kuongezeka. "Hatuwezi kusafirisha kwa ndege idadi hii yote ya majeruhi (...). Tunaomba yeyote anayeweza kututumia msaada afanye hivyo", aliongeza mkuu wa nchi, baada ya yeye mwenyewe kuchangia kutoa damu yake kwa ajili ya huduma kwa majeruhi.

Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre ameamuru shule zifungwe ili wanafunzi waweze kuchangia damu.

Vita vya muda mrefu

Somalia na "magaidi hawa wako vitani", Rais Hassan Sheikh Mohamud pia alisema. Kulingana na rais wa Somalia, shambulio hili linaonyesha kwamba Waislam wa Al-Shabab "wamepoteza na (...) hawawezi kukabiliana na jeshi, kwa hivyo waliingia kisiri na kuwaua raia wasio na hatia".

Shambulio hilo lilifanyika katika njia panda ambazo tayari ilikumbwa na shambulio baya zaidi kuwahi kufanywa nchini Somalia: watu 512 waliuawa Oktoba 14, 2017 kwa mlipuko wa lori lililokuwa limebeba vilipuzi. Ali Yare Ali, afisa katika mji wa Mogadishu, amewaambia waandishi wa habari kuwa kati ya miili 7 na 9 imekwama chini ya vifusi.

Jumuiya ya kimataifa imelaani haraka shambulio hilo. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia umeahidi kusimama "kwa uthabiti na Wasomali wote dhidi ya ugaidi" na Washington ikalaani shambulio la "chuki" na kuzihakikishia mamlaka za Somalia "uungaji mkono wao katika mapambano ya kuzuia mashambulizi hayo ya kigaidi".

Kundi la wanamgambo la Al Shabab lenye mafungamano na Al-Qaeda limekuwa likipambana na serikali ya shirikisho inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa tangu mwaka 2007. lilitimuliwa kutoka Mogadishu mwaka 2011 lakini imesalia kuwa imara katika maeneo makubwa ya vijijini, hasa kusini mwa nchi, na mara kwa mara hufanya mashambulizi katika mji mkuu na miji mikubwa ya Somalia.

Katika miezi ya hivi karibuni, Al Shabab wameongeza maradufu harakati zao nchini Somalia, nchi maskini na isiyo na utulivu katika Pembe ya Afrika, na hasa shambulio la kushangaza, lililochukua karibu saa thelathini, mwishoni mwa mwezi wa Agosti dhidi ya hoteli moja huko Mogadishu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.