Ghana: Zaidi ya kumi na sita waangamia katika mlipuko katika eneo la madini la Bogoso
Ghana inaomboleza vifo vya raia wake zaidi ya 16 waliofariki dunia katika mlipuko uliosababishwa na ajali baada ya gari kadhaa kugongana.
Imechapishwa:
Lori lililokuwa limebeba vilipuzi lililipuka baada ya ajali ya barabarani, Alhamisi, Januari 20, magharibi mwa nchi. Ripoti rasmi ya kwanza inabaini kwamba watu 17 wamefariki dunia na 59 kujeruhiwa, baadhi yao wakiwa katika hali mbaya.
Ripoti ya kwanza iliyotolewa na mamlaka ya Ghana unabaini kwamba ajali hiyo ilisababishwa na lori lililojaa vilipuzi kugongana na magari mengine katika eneo la Apiate.
Mlipuko huo ulitokea mwendo wa saa sita mchana siku ya Alhamisi huko Apiate, sio mbali na Bogoso, mji wa kunakochimbwa madini ulioko kilomita 300 magharibi mwa Accra, mji mkuu.
Kulingana na picha za shirika la habari la AFP, ajali hiyo na mlipuko vimesababisha uharibifu mkubwa huku katika eneo la tukio kukionekana miili ya watu ambao hawakuweza kutambuliwakulinganana mashahidi.
Kwa mujibu wa ripoti ya kwanza ya uchunguzi, ni "ajali iliyohusisha lori lililokuwa likisafirisha vilipuzi kwa kampuni ya uchimbaji madini, pikipiki na gari la tatu iliyotokea karibu na transfoma ya umeme na kusababisha mlipuko huo," alisema Waziri wa Habari, Kojo Oppong-Nkrumah, katika taarifa iliyotolewa usiku wa Alhamisi kuamkia Ijumaa na kuripotiwa na shirika la habari la AFP.
Hospitali zote zilizo karibu na eneo la tukio zimewapokea majeruhi na kumeanzishwa mpango wa kuwahamisha walio katika hali mbaya hadi mji mkuu Accra.
Alhamisi alasiri, Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo, alisikitishwa na "tukio baya, la kusikitisha na la kuhuzunisha" na kutoa rambirambi zake kwa familia za wahanga.