Pata taarifa kuu
DRC-SIASA

Hatma ya mazungumzo ya kitaifa nchini DRC mashakani

Mazungumzo ya kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, ambayo yalitarajiwa kuendelea Ijumaa ya September 23 yanaelekea kukwama baada ya washiriki wa mazungumzo hayo kutangaza kujiondoa, kikiwemo chama cha Vital Kamerhe.

Kiongozi wa upinzanik nchini DRC anayeshiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa, Vital Kamerhe, sasa amejiondoa kwa muda
Kiongozi wa upinzanik nchini DRC anayeshiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa, Vital Kamerhe, sasa amejiondoa kwa muda www.politico.cd
Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa upinzani kwenye mazungumzo hayo Vital Kamerhe amesema kuwa uamuzi huo unafuatia mauaji yaliyojitokeza wakati wa maandamano ya juma hili pamoja na uharibifu wa miundombinu na makao makuu ya vyama.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamerhe ametoa pia salamu za rambirambi kwa familia za watu waliopoteza maisha ambapo kwa mujibu wa polisi na serikali idadi yao ni 32 huku upinzani unaoongozwa na Tshisekedi wa mulumba ukitaja idadi ya watu wasiopungua 100.

Kabla ya upinzani, kanisa katoliki na lenyewe limetangaza kujiondoa kwenye mazungumzo hayo likifuatiwa na shirika la raia la “La Voix des Sans Voix” kwa sababu hiyohiyo hatua ambayo imemweka kwenye wakati mgumu mratibu wa mazungumzo hayo, Edem Kodjo.

Hata hivyo, bado upinzani kwa ujumla wake unataka upande wa serikali kuzingatia masharti yake kabla ya kusaini makubaliano yoyote ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kuheshimu katiba na azimio namba 2277 la umoja wa mataifa, kutajwa kwa tarehe ya uchaguzi na hatma ya rais Kabila ifikapo tarehe 19 Desemba mwaka huu.

Sanjari na hayo, uboreshwaji wa daftari la wapiga kura nao unatakiwa kuchukua muda mfupi pamoja na kuundwa upya kwa Tume huru ya Uchaguzi CENI, inayosadikiwa kutumika kwa maslahi ya rais Joseph kabila.

Katika muktadha huo, ni vigumu kufikia makubaliano yaliyotarajiwa mwishoni mwa juma hili kama jawabu kwa mgogoro wa Congo ambao kwa sasa umeanza kuchukua mkondo wa pambano la kisiasa kumuondoa rais madarakani ili katiba iheshimiwe.

Hapo Jana mabalozi wa kimataifa nchini DRC walimtembelea Etienne Tshisekedi ambaye alikuwa na vinara wengine wa Upinzani, ambapo taarifa za ndani zinasema kuwa wanadiplomasia hao walimuomba wajiepushe na vurugu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.