Pata taarifa kuu
NGUMII-FURY

Bodi ya masumbwi nchini Uingereza yazuia kwa muda leseni ya bondia Tyson Fury

Leseni ya kupigana ya bondia wa Uingereza, Tyson Fury, imezuiliwa kwa muda ikiwa ni siku moja tu imepita toka mwanamasumbwi huyu atangaze kuachia mikanda yake yote ya uzito wa juu kutokana na matatizo ya afya ya akili.Bodi inayosimamia na kudhibiti mchezo wa masumbwi nchini Uingereza, imethibitisha kusitishwa kwa muda kwa leseni ya bondia huyo ili kutoa nafasi zaidi ya kufanyika uchunguzi kuhusu tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli na matatizo ya kiafya aliyonayo.

Bondia Tyson Fury akiwa na mataji yake, Novemba 28, 2015
Bondia Tyson Fury akiwa na mataji yake, Novemba 28, 2015 Reuters / Lee Smith Livepic
Matangazo ya kibiashara

Mwezi Juni mwaka huu, shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini Uingereza, ilimshtaki Fury kwa tuhuma za kutumia dawa zilizopigwa kutumiwa michezoni.

Haya yanajiri wakati ambapo Jumatano ya wiki hii, bondia huyo alitangaza rasmi kuachia mataji yake mawili ya uzito wa juu ya WBO na WBA, akisema anatumia muda huu kufanya matibabu ya kiafya.

Fury mwenye umri wa miaka 28 hivi sasa, juma moja lililopita alikiri kutumia dawa za kulevya aina ya Cocaine kukabiliana na hali ya msongo wa mawazo aliokuwa nao, ambapo sasa huenda akapoteza pia leseni yake ya masumbwi.

Fury hajapigana toka alipomshinda Wladimir Klitschko mwezi November mwaka jana na ambapo kwa zaidi ya mara mbili alitangaza kujitoa kurudiana na Klitschko.

“Kwa mara nyingine nimeingia katika changamoto kubwa ya maisha yangu, ambayo najua ni kama nilivyomshinda Klitschko na ndivyo nitakavyoshinda hali hii.” alisema bondia huyo.

Tyson Fury, akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni
Tyson Fury, akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni Reuters / Alex Morton

Fury alisema kuwa ni kwa nia njema ya mchezo wa masumbwi na kwamba ni haki na halali kuikabidhi mikanda hiyo kushindaniwa kwenye ulingo.

“Nilishinda mataji haya kwenye ulingo na naamini yanapaswa kushindaniwa kwenye ulingo, lakini kwa sasa siwezi kutetea mataji yangu na nimeamua kuchukua uamuzi mgumu na wenye hisia kuamua rasmi kuyaacha mataji yangu.” alisema Fury.

Kwenye taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari, promota wa Fury, Hennessy Sports amesema kuwa uamuzi huu utamruhusu Fury kupata muda wa kutafakari na kujitathmini wakati huu akiendelea kupata matibabu kamili bila kuwa na shinikizo lolote.

Mick Hennessy aliongeza kuwa uamuzi uliochukuliwa na Fury “Unaumiza moyo”.
Mjomba na mkufunzi wa Fury, Peter Fury amesema kuwa mchezaji wake atarejea kwa nguvu na kuchukua tena mataji yake aliyokuwa akiyamiliki kiuhalali.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.