Pata taarifa kuu
BURUNDI-UCHAGUZI-SIASA

Wananchi wa Burundi watakiwa kuchangia fedha za uchaguzi wa 2020

Serikali ya Burundi imewatolea wito raia wake kuchangia bila kulazimishwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Pascal Barandagiye, mchango huo unatolewa kwa hiari wala sio kulazimishwa.

Serikali ya Burundi inasema raia watakiwa kuchangia kwa hiari yao katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Serikali ya Burundi inasema raia watakiwa kuchangia kwa hiari yao katika uchaguzi wa mwaka 2020. PHOTO / PHIL MOORE
Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Fedha zilitoa siku ya Jumatatu (Desemba 11) agizo linaloelezea jinsi ya kukusanya mchango wa raia wa Burundi kwa uchaguzi ujao.

Mchango utatolewa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari 1, 2018. Wachangiaji wamewekwa katika makundi matatu. Wananchi ambao si wafanyakazi wa serikali watatoa mchango wa Faranga za burundi 2,000 ( sawa na nusu ya dola 1) kwa kila mwaka kwa kila familia na Franaga za Burundi 1,000 kwa mwaka kwa wanafunzi walio na umri wa kupiga kura.

Mchango kwa watumishi wa umma utatolewa kwa kiwango cha mishahara yao. Wale wanaolipwa mishahara hadi Faranga za Burundi 50,000 Fbu kwa mwezi watachangia Faranga 500 kila mwezi. Wale ambao mshahara yao ni kati ya Faranga 50, 001 na 100, 000 watatoa mchango wa kila mwezi wa Faranga 1000. Kulingana na agizo hilo mtumishi wa umma, ni mtu yeyote anayefanya kazi katika ofisi, kampuni, na shirika la serikali, ikiwa ni pamoja na wabunge na wanaseneta na wafanyakazi katika mabunge yote mawili, viongozi na wafanyakazi serikalini, wanadiplomasia wa Burundi, vikosi vya ulinzi na usalama. Kwa yule ambaye mshahara wake uko kati ya Faranga 100 001 na 200,000 atachangia Faranga 2,000 kwa kila mwezi. Mchango wa 5,000 kwa kila mwezi utatolewa kwa yule anayepata mshahara kati ya Faranga 200,001 na 500,000 . Yule anayepata mshahara kati ya Faranga 500,001 na milioni moja , atatoa mchango wa Faranga 30,000 kwa mwezi. Kwa wale ambao mishahara yao ni zaidi ya 1,000,000 Fbu, michango yao itakuwa mshahara wa mwezi mmoja kwa mwaka.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani Pascal Barandagiye amesema kuwa mtumishi wa umma ambaye hatachangia atatakiwa atoe maelezo kwa barua na kuwasilisha barua hiyo kwa viongozi husika.

Wadadisi wanasema hata kama serikali imetangaza kwamba mchango huo unatolewa na raia yeyote wa Burundi kwa hiari yake, kuna hatari watu ambao watakua hawakuchangia katika uchaguzi huo wakose baadhi ya huduma kutoka ofisi za serikali, na hali hiyo inaweza kuwa miongoni mwa njia za kukuza au kuendeleza utawala wa kimla nchini humo.

Burundi inaendelea kukabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Ulaya na Marekani, ambao ni wafadhili wa kubwa wa taifa hilo dogo la Afrika ya Kati, kufuatia msimamo wa serikali wa kukataa mazungumzo na upinzani na kuendelea kuvunja haki za binadamu.

Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, asilimia kubwa ya wananchi wa Burundi wanakabiliwa na hali duni ya maisha, na itakua ni vigumu kwao kuchangia ili kupatikane kiwango cha kutosha kwa minajali ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Burundi ni miongoni mwa nchi masikini duniani na wafadhili wakubwa ni nchi za Ulaya na Marekani, ambapo mchango kutoka nje ni sawa na asilimia 47.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.