Kenya yahifadhi ubingwa wa mashindano ya Tong-Il Moo-Do kwa mara ya 11
Mombasa, Kenya – Timu ya taifa ya Kenya mchezo wa Tong-Il Moo-Do, Jasiri imehifadhi taji la Mombasa Open kwa mara ya 11 katika mashindano yaliyokamilika siku ya Jumanne katika ukumbi wa Akademia ya Agha Khan jijini Mombasa nchini Kenya.
Imechapishwa:
Kenya ilishinda kwa jumla ya medali 191 ambayo ni medali 10 zaidi ya waliyopata katika mashindano ya mwaka jana. Kati ya 191 - 46 ni za dhahabu, 52 za fedha na 93 za shaba kwenye vitengo tofauti.
Nahodha wa Jasiri Elvis Malupe akizungumza na Rfi Kiswahili Michezo, alionesha furaha yake huku akitoboa siri ya muendelezo wa ushindi wa taji hilo.
Sisi kama Jasiri tumeonesha ujasiri wetu tukatetea taji letu. Tulihakikisha tuna wachezaji katika kila kitengo na ni wachezaji ambao wamebobea kwenye mchezo huu.
Rais wa shirikisho hilo nchini Kenya, Clarence Mwakio aliipongeza timu ya taifa kwa juhudi walizoonesha bila kusahau ufadhili wa dola elfu 646.4 waliopata kutoka kwa serikali kuu kupitia wizara ya michezo nchini Kenya chini ya waziri Ababu Namwamba.
Tulitarajia timu 42 lakini tukabahatika kupata 13, tukisonga mbele tunatarajia kuwa na mashindano mengi bora zaidi kuliko haya ambayo yataweza kukuza vipaji, mchezo huu hapa Kenya na Afrika kwa jumla.
Aidha rais aligusia uwezekano wa kuandaa mashindano ya Mombasa Open mwezi Agosti kutoka mwezi Disemba kama ambavyo imekuwa kwa miaka iliyopita, kutokana na ukosefu wa ndege za usafiri kuingia Kenya wakati huu wa msimu wa utalii.
DRC ilimaliza nafasi ya tisa kwa medali moja tu, Zambia ikimaliza ya tatu kwa medali 23 (10 za dhahabu, 5 za fedha na 8 za shaba). Mataifa mengine ya Afrika, Nigeria ilishikilia nafasi ya saba kwa medali nne - mbili za dhahabu na mbili za shaba nayo Cote D'Ivoire ikivuta mkia bila medali yoyote.
Ufilipino ilikuwa ya tatu kwa medali 11.
'Yaliyopita si ndwele ...'
Nahodha Elvis Malipe tayari analenga kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya dunia ya mwaka 2024 yatakayofanyika nchini Ufilipino.
Ushindi huu unatutambulisha kama watu wa kuogopewa. Timu zingine zijitayarishe kwa upinzani mkali sana.
Kenya ilishiriki Mashidano ya Dunia ya Tong-Il Moo-Do mara ya mwisho mwaka 2019 nchini Korea Kusini na ikamaliza nafasi ya pili.
Tunalenga kupeleka timu kubwa sana Ufilipino kwa vile timu ya Ufilipino ina upinzani mkuu, lazima tuende kama tumejipanga vilivyo kupabana.
Kwenye hotuba yake rais Clarence Mwakio, alitaja umuhimu na nia ya mataifa ya Afrika kuanzisha mpango wa ufadhili wa masomo ya wachezaji kama njia mojawapo kuu ya kukuza mchezo huo barani Afrika.