Pata taarifa kuu
Tong-Il Moo-Do

Erica de Sequeira kutoka India asifia wachezaji wa Afrika ukumbini

Mombasa, Kenya – Kinda wa miaka 13 kutoka Goa nchini India, Erica de Sequeira ametoa sifa sufufu kwa wachezaji wa Kenya na bara nzima la Afrika akisema wameimarika na ni wenye upinzani mkali ukumbini wakati wa mechi za Tong-Il Moo-Do za mashindano ya kimataifa inayoendelea jijini Mombasa nchini Kenya.

Erica de Sequeira baada ya kushinda dhahabu yake ya kwanza kwenye Mombasa Open 2023
Erica de Sequeira baada ya kushinda dhahabu yake ya kwanza kwenye Mombasa Open 2023 © Jason Sagini
Matangazo ya kibiashara

Erica ambaye anaorodheshwa nafasi ya tatu ulimwenguni, alikuwa akizungumza siku ya Jumatatu jioni baada ya kumlemea mkenya Eunice Mwende 3:2 katika pambano la sparring na hivyo basi kuishindia India dhahabu ya kwanza kwenye mashindano.

Timu ya India yenye wachezaji wawili tu katika toleo la mwaka huu ni miongoni mwa mataifa yanayoshiriki mashindano hayo.

Mataifa ya Afrika yanayoshiriki ni - Kenya, DRC, Congo Brazaville, Zimbabwe na Zambia. 

Tumekua mazoezini kwa muda sasa, nimewaona wachezaji wa Afrika ukumbini. Lazima nikiri kuwa wameimarika sana ukumbini wakati wa mazoezi na kwenye mechi.

Erica ambaye alianza kucheza mchezo huu akiwa na umri wa miaka tisa tu anajivunia medali kadhaa za kimataifa pamoja na kushiriki mashindano makubwa ulimwenguni. Alishinda medali nne (mbili za dhahabu na mbili za fedha) katika makala ya mwaka 2022 ya Mombasa Open Tong-Il Moo-Do. 

Erica baada ya kushinda dhahabu kwenye toleo la 10 mashidano ya Mombasa Open Tong-IL Moo-Do mwaka 2022.
Erica baada ya kushinda dhahabu kwenye toleo la 10 mashidano ya Mombasa Open Tong-IL Moo-Do mwaka 2022. © Kenya Tong Il Moo Do Federation media

Wachezaji wa Kenya ni simba wa mechi lakini mimi ni simba mfalme wa mechi kwa hivyo kulingana na mawazo yangu nafanya mazoezi vizuri na hakuna anayeweza kunishinda.

Aliweka historia mwaka 2022 kuwa mshindi mwenye umri mdogo zaidi katika sanaa ya vita kutoka India na msichana wa kwanza pekee kutoka India ambaye kwa mara ya kwanza alishiriki na kushinda medali ya shaba katika mashindano ya Kamati ya Umahiri ya Dunia (WMC).

Mwaka uo huo mwezi Julai, aliiwakilisha India kwenye Kombe la Dunia jijini Istanbul, Uturuki. Kwa mara ya kwanza alishinda medali ya fedha na shaba katika mashindano ya Dunia ya Tong-Il Moo-Do yaliyofanyika Korea Kusini mwaka wa 2021. 

Kocha wake Raunak Singh ndiye humtia moyo katika uchezaji na pia kucheza densi ya mziki wa kizazi kipya wakati wa sherehe za ufunguzi wa mashindano ya sanaa ya kupigana. Wazazi wa msichana huyu anayesoma shule ya upili pia ni wenye nguzo muhimu katika ukuzaji wa talanta yake. 

Ni mchezaji ambaye hupokea upendo mwingi anaposimama ukumbini na hili ni jambo ambalo anasema humsaidia kupata nguvu zaidi ili kunawiri kwa kujituma zaidi. 

Erica akiwa mazoezini
Erica akiwa mazoezini © ericadesequeira instagram

Erica ambaye alikosa kushiriki toleo la kumi la Mombasa Open kufuatia ukosefu wa ufadhili wa fedha na vizuizi vya virusi vya Covid-19, anasema anaupenda mchezo huo kwani ni chombo cha kuleta watu pamoja.

Katika mashindano ya mwaka huu ya Mombasa Open, anasema analenga kushinda dhahabu tu kwenye vitengo atakavyoshiriki.

Ninaamini katika mafunzo ya makocha wangu na ninaamini kuwa ninaweza kufanya hivyo.

Erica ambaye pia ni mchezaji wa Jujitsu, anasema analenga kushiriki mashindano makubwa duniani kama vile michuano ya Shirikisho la Kimataifa la Jiu-Jitsu la Brazili na michezo ya Olimpiki. Kwenye Tong-Il Moo-Do, analenga kuwa mchezaji bora zaidi ulimwenguni na kucheza katika Kombe la Amani la dunia. 

Kama si Tong-Il Moo-Do au Jiu-Jitsu basi nadhani ningekuwa mchezaji wa basketboli.

Hadi kufikia sasa, Kenya inaongoza jedwali kwa jumla ya medali 24 (dhahabu nane, fedha tano na shaba 11), India ni ya pili ikifuatwa na Iran kisha Zambia - kila moja ikiwa na medali moja. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.