Pata taarifa kuu
WAFCONQ 2024

Mechi ya kufa kupona kwa Kenya dhidi ya Cameroon

Nairobi – Timu ya taifa ya Kenya ya wasichana walio chini ya miaka ishirini imekamilisha mazoezi yake ya mwisho leo asubuhi kabla ya mchezo wa marudiano kesho dhidi ya Cameroon katika awamu ya tatu ya kufuzu Kombe la Dunia la mwaka 2024.

Kocha wa Kenya U20 Beldine Odemba kwenye mazoezi
Kocha wa Kenya U20 Beldine Odemba kwenye mazoezi © Football Kenya Federation
Matangazo ya kibiashara

Kocha wa timu ya Kenya ‘Rising Starlets’ Beldine Odemba ametangaza vita dhidi ya Cameroon huku wakilenga ushindi wa angalau mabao manne kwa bila ili kufuzu raundi ya mwisho baada ya kupoteza mabao 3-0 kwenye mkondo wa kwanza uliochezwa wikendi iliyopita katika uwanja wa Ahmadou Ahidjo jijini Yaounde, Cameroon.

Soka ni vita, kila mashindano ni vita. Ukienda vitani, hutoki ukisema unaenda kufa. Kila mtu huenda kujizuia na kutumai atarejea nyumbani akiwa hai. Bado tuna nafasi ya pili kufuzu, amesema kocha Beldine Odemba.

Kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Cameroon, Kenya ilikosa huduma za wachezaji nane ambao wanaendelea na mtihani wao wa kidato cha nne, lakini kocha Beldine anasema wachezaji walioitwa kujaza nafasi zao wanaendelea vizuri.

Shida kubwa ilikuwa kuwaweka pamoja na kushikana kama timu lakini kwa sasa wamejifunza mambo kadhaa na wameimarika vilivyo. Hatujakuwa na mechi yoyote ya kirafiki lakini utaona tofauti kwenye mazoezi na kwenye mchezo kesho, Beldine Odemba.

Kocha Beldine ametaja umuhimu wa mashabiki uwanjani kuipa timu hiyo motisha katika harakati ya kugeuza matokeo akitoa mfano wa wakati timu ya taifa ya kina dada Harambee Starlets iliibandua Cameroon kwenye michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kina dada kwa njia ya ya penalti mwezi Septemba katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya.

Kaimu nahodha wa Kenya, Rebecca Kwoba amesisitiza maneno ya mwalimu Odemba akidai wanahitaji kujiamini zaidi na kuwa wana imani watashinda mchezo na kufuzu raundi ya mwisho ambapo watakutana na mshindi kati ya Misri na Congo.

Tunawaomba mashabiki waje kwa wingi sababu uwepo wao utatupa msukumo maradufu. Mazoezi yamekua mazuri na kesho tutafunga hayo magoli manne na tufuzu, alitamka Rebecca Kwoba kwa kujiamini.

Wachezaji wa Rising Starlets wakiwa mazoezini awali
Wachezaji wa Rising Starlets wakiwa mazoezini awali © Football Kenya Federation

Uchanganuzi wa Cameroon

Kocha wa Kenya amefichua kuwa wamefanya kazi ya ziada kwa kuangalia video za awali za wapinzani wao pamoja na mechi ya mkondo wa kwanza.

Tumefanya uchambuzi wetu na tumeona tulipokosea na wapi walitulemea.

Kocha wa Cameroon Hassan Balla anafahamu uwezo wa Kenya akilenga ushindi kwenye mchezo huo.

Kesho tunacheza mechi mpya ambayo haina uhusiano kabisa na ushindi wa 3-0 kwenye mkondo wa kwanza. Kenya ina wachezaji wazuri na mchezo wao unapendeza lakini tutazingatia sana tuliyofanya kwenye mazoezi kutafuta ushindi, alisisitiza kocha wa Cameroon.

Matukio ya mwezi Septemba yangali kwenye kumbukumbu ya timu ya chipukizi ya Cameroon, beki Marlene Essimi ameeleza athari ya matokeo hayo.

Itatuathiri ndio lakini pia inatutia motisha ila ilituumiza sana. Kesho tutajituma ili kubadilisha matokeo yaliyopita, alisikitika Marlene Essimi.

Kombe la Dunia la kina dada walio chini ya umri wa miaka ishirini litaandaliwa nchini Colombia mwezi Agosti mwaka ujao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.