Pata taarifa kuu

Kocha wa URA ya Uganda Sam Timbe afariki dunia

Nairobi – Na  Jason Sagini

Kocha wa URA SC ya nchini Uganda, Sam Timbe ameaga dunia
Kocha wa URA SC ya nchini Uganda, Sam Timbe ameaga dunia © URA SC
Matangazo ya kibiashara

Kocha wa URA SC ya nchini Uganda, Sam Timbe ameaga dunia. Mtaalamu huyo mkongwe amefariki wakati akipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi mapema leo.  

“Tunasikitika kuwaarifu kwa bahati mbaya ya kuondokewa na mheshimiwa Kocha wetu Mkuu, Sam Timbe, mchana wa leo alipokuwa njiani kuelekea hospitali ya Nakasero kwa ajili ya matibabu, baada ya kupewa rufaa na hospitali ya St Catherine. Tunatuma salamu za rambirambi kwa familia na wapendwa wake katika kipindi hiki kigumu cha maisha. Kwa sasa, timu yetu iko kambini katika hoteli ya Standard, Kampala, ikijiandaa na mchezo ujao wa nusu fainali ya kombe la FUFA Super 8 dhidi ya KCCA FC, uliopangwa kesho katika uwanja wa MTN Omondi. Taarifa zaidi itatolewa kwa wakati ufaao," sehemu ya taarifa kutoka kwa klabu ya URA unasomeka. 

Sam Timbe pia amewahi kuwa kocha kwenye klabu ya Tusker FC na Sofapaka FC nchini Kenya. 

Timbe alijiunga na Tusker Januari 2018 baada ya klabu hiyo kuachana na Mganda mwingine George 'Best' Nsimbe. Hata hivyo alikaa kwa muda mfupi kwani alitimuliwa baada ya mechi 11 pekee kufuatia msururu wa matokeo duni. 

Timbe alishinda Ligi kuu ya soka nchini Kenya akiwa na Sofapaka mwaka 2014 kabla ya kuhamia Police FC inayoshiriki Ligi Kuu ya soka nchini Uganda. 

Rekodi zake nyingine bora katika maisha yake ya soka ni pamoja na kushinda mataji ya ligi akiwa na SC Villa ya Uganda, Atraco ya Rwanda na Young Africans ya Tanzania. 

Kazi yake pia ilizaa matunda katika michuano ya CECAFA Kagame Cup kwa kulinyanyua taji hilo mara nne akiwa na timu mbalimbali na kuwa mmoja wa makocha mahiri Afrika Mashariki. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.