Australia imewaondoa Ufaransa kwenye kombe la dunia
Nairobi – Australia sasa itamenyana na washindi wa mchujo wa mwisho wa nane bora kati ya Uingereza na Colombia baada ya kuwashinda ufaransa katika mechi ya kuwania ubingwa wa dunia upande wa wanawake.
Imechapishwa:
Baada ya sare ya 0-0 katika mda wa dakika 120, mechi hiyo iliingia katika hatua ya penalti, Cortnee Vine akifunga penalti ya ushindi baada ya timu zote kupiga mikwaju 10.
Vicki Becho alikosa penalti ya 10 ya Ufaransa, na ikasalia kwa Vine kuivusha Australia kwa kumshinda kipa wa akiba wa Ufaransa, Solene Durand. Pambano hilo lilitazamwa na umati wa watu 49,461.
Les Bleues walikuwa na matumaini ya kufika nusu fainali kwa mara ya pili, kufuatia kushindwa katika mechi nne za mwisho mwaka 2011, lakini badala yake wamerudi nyumbani.
Kocha wa Australia, Matildas Tony Gustavsson alisalia na timu ile ile iliyoanza dhidi ya Denmark katika hatua ya 16 bora, huku Ufaransa ikimrejesha kwenye safu ya ulinzi Maelle Lakrar.
Tayari timu zote za bara Afrika zimeyaaga mashindano huku bara Ulaya likiwa limesalia na wawakilishi 3 ambapo tayari Sweden na Uhispania watakutana katika nusu fainali ya kwanza.
Taifa lingine la bara Ulaya Uingereza wanakabiliana na Colombia katika mchezo wa robô fainali.
Bingwa mtetezi Marekani katika Makala mwaka 2019 yaliyoandaliwa nchini Ufaransa, ameondolewa katika mashindano ikiwa na maana sasa makala ya mwaka huu yatakuwa na bingwa mpya.