Riyad Mahrez na Henderson Kuhamia Saudi Arabia
Nairobi – Manchester City wamekubali kumuuza winga wao wa kulia Riyad Mahrez katika klabu ya Al-Ahli kwa ada ya pauni milioni 30.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Tayari mchezaji huyo wa kimataifa wa Algeria mwenye umri wa miaka 32 ameachiliwa na Manchester City wanaojiandaa kwa msimu mpya nchini Korea Kusini na Japan.
Klabu ya Al-Ahli yenye maskani yake Jeddah tayari imemsajili Roberto Firmino baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Liverpool na kipa Edouard Mendy kutoka Chelsea katika msimu wa mbali.
Mwananchi mwenzake Mahrez, Ryad Boudebouz alijiunga na Al-Ahli Septemba mwaka jana.
Mpinzani wa kihistoria wa Manchester, Liverpool, anajenga upya safu yake ya kiungo.
Msimu huu wa joto, The Reds walileta Alexis Mac Allister na Dominik Szoboszlai hili kuimarisha safu yao ya kati.
Jürgen Klopp anatazamiwa kupoteza kiungo mwingine muhimu wa timu yake ambaye ni Jordan Henderson.
Jordan Henderson anakaribia kuondoka kwenye kikosi hicho, kwani Liverpool wamefikia makubaliano na Al Ettifaq.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza anatazamiwa kusaini mkataba wa miaka 3 na klabu hiyo ya Saudia.
Henderson mwenye umri wa miaka 33, ambaye amesalia na miaka miwili kwenye mkataba wake Anfield, alikuwa Ujerumani na Liverpool kwa kambi yao lakini hakushiriki katika mchezo wao wa kwanza wa kujiandaa na msimu dhidi ya Karlsruher.
Pia alikosekana kiungo mwenza Fabinho, ambaye klabu hiyo ilipokea ofa ya pauni milioni 40 kutoka kwa Al-Ittihad siku ya Ijumaa.
Nahodha wa zamani wa Liverpool Steven Gerrard aliteuliwa hivi karibuni kuwa meneja wa Al-Ettifaq jambo ambalo linachangia uhamisho mkubwa wa mastaa wa Liverpool.