Rais wa PSG Al-Khelaifi asifia viwango vya soka Afrika
NAIROBI – Na Paul Nzioki
Imechapishwa:
Rais wa klabu ya Paris Saint-Germain, Nasser al-Khelaifi, amesisitiza dhamira yake katika soka la Afrika baada ya kushuhudia fainali kati ya Al Ahly ya Misri na Wydad ya Morocco katika kombe la klabu bingwa barani Afrika.
Al-Khelaifi ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Vilabu Ulaya (ECA) ameongeza kusema kuwa kuna nia ya kuvipa vilabu vya Afrika rasilimali ndio viimarike zaidi.
Katika mahojiano na beIN Sports, al-Khelaifi alipongeza mchezo wa timu zote mbili na kuwataka watazamaji kutodharau kiwango cha soka barani Afrika.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyu ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa shirika la Habari la beIN, bara Afrika kwa muda mrefu limekuwa likijulikana kwa wachezaji wake mahiri na mechi za kusisimua zisizotabirika.
"Tunathibitisha dhamira yetu ya kuipa soka la Afrika msaada unaohitajika ili kufikia uwezo wake kwa kuiwezesha kukuza vipaji vyake na kuipatia rasilimali muhimu," alisema na kuongeza kuwa soka sio tu kushinda ubingwa, bali pia kuinua ubinadamu kwa kiwango cha kimataifa.
"Leo, tunaendelea kuweka mipango ambao unapita zaidi ya jukumu la mpira wa miguu kwa maendeleo ya jamii zote ulimwenguni. Wakati wa Mkutano Mkuu uliopita wa ECA, tulichambua tu kile ambacho ECA inaweza kutimiza, na tunatazamia sura inayofuata. ECA ya siku zijazo itakuwa na ushawishi sio tu barani Ulaya, bali pia kote ulimwenguni, pamoja na Afrika.
Al-Khelaifi alimshukuru Fouzi Lekjaa, Rais wa Shirikisho la Soka la Kifalme la Morocco, na watu wa Morocco kwa ujumla kwa ukarimu wao, akiongeza kuwa umati huo wa watu wenye hamasa ulimvutia.
Katika Fainali hiyo Al Ahly ilishinda ubingwa wake wa 11 karika ardhi ya Afrika na kuendeleza rekodi yake y akua klabu bora barani afrika mda wote kwa idadi ya mataji.