Pata taarifa kuu

Tenisi : Okutoyi kuongoza kikosi cha Kenya kwenye mashindano ya Billie Jean King

Na: Jason Sagini

Mchezaji wa Kenya, Angella Okutoyi
Mchezaji wa Kenya, Angella Okutoyi © @OLIVER ANANDA
Matangazo ya kibiashara

Bingwa wa mashindano ya Wimbledon mwaka 2022 kitengo cha wachezaji wawili, Angella Okutoyi ataongoza kikosi cha Kenya kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la kina dada daraja la tatu barani Afrika.

Mashindano hayo yatafanyika nchini Kenya kuanzia Juni 12-17 katika uwanja wa Nairobi Club na kuwakutanisha wachezaji kutoka mataifa 12.

Okutoyi mwenye umri wa miaka 19, anayesoma nchini Marekani, atashirikiana na pacha Roselida Asumwa na Alicia Owegi pamoja na Cynthia Cheruto.

“Nimezoea kushiriki mashindano ya kimataifa nje ya taifa na bara letu. Wakati huu shinikizo ni kubwa sababu nacheza nyumbani,” amesema Okutoyi.

Asumwa, Owegi na Cheruto walimaliza nafasi ya kumi na moja kati ya mataifa 14 baada ya kupoteza seti 2-0 dhidi ya Botswana kwenye hatua ya mtoano.

Kikosi cha wachezaji wa Kenya
Kikosi cha wachezaji wa Kenya © ALL RIGHTS RESERVED @OLIVER ANANDA

Aidha, kikosi hicho chini ya kocha Francis Rogoi, Stacy Yego na Melissa Mwakha mwenye makaazi yake nchini Zimbabwe wametajwa kama wachezaji wa akiba.

“Maandalizi yanaendelea vizuri hadi sasa timu ikiwa kwenye kambi ya mazoezi ya Nairobi Club,” amesema Wanjiru Mbugua msimamizi wa mashindano hayo na katibu mkuu wa Shirikishi la mchezo wa Tennis nchini Kenya.

Kocha wa timu hiyo Francis Rogoi, anasema ana matumaini makubwa kuwa, kikosi hicho kitafanya vizuri kwenye mashindano hayo.

“Tuliwachagua kikosi kwa kuzingatia uzoefu, nidhamu, bidii ya mchezaji na kiwango cha uchezaji,” amesema.

Kenya ilishiriki kombe la Billie Jean King mara ya kwanza mwaka 1991 hadi mwaka 2005 kisha kujiondoa na kurejea tena mwaka 2012.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.