Pata taarifa kuu

Tenisi: Taji la Billie Jean King kuandaliwa Nairobi, Juni 12-17.

Na: Jason Sagini

Uwanja wa mchezo wa Tennis
Uwanja wa mchezo wa Tennis © AFP - MARTIN BUREAU
Matangazo ya kibiashara

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995, Kenya itakuwa mwenyeji wa mashindano ya tenisi  ya Kombe la dunia kwa wanawake kwenye daraja la tatu barani Afrika kuanzia Juni 12-17 jijini Nairobi katika uwanja wa Nairobi Club.

Mashindano haya yanaitwa Billie Jean King Cup kwa heshima ya mchezaji wa tenisi kutoka Marekani (Billie Jean King) aliyeshinda jumla ya mataji 39 katika taaluma yake ya uchezaji.

Awali kombe hili liliitwa Fed Cup kuanzia mwaka 1995 kisha kubadilishwa jina Septemba mwaka 2020 na kuitwa Billie Jean King Cup.

Tayari viwanja tisa vya udongo vipo kwenye hatua za mwisho za ujenzi, hii ikiwa mojawapo ya mabadiliko yatakayoshuhudiwa nchini Kenya kwani viwanja hivi havijawahi kutumika ikiwa ndio mtindo wa mashindano makubwa ya tenisi duniani. Mashindano haya pia ni sehemu ya kufuzu kwa Olimpiki ya mwaka 2024 jijini Paris, Ufaransa.

Mataifa kumi na mbili yatapigania tiketi moja tu ya kupandishwa ngazi hadi daraja la pili barani Afrika wakati atakayevuta mkia atashushwa ngazi hadi daraja la nne.

 

Morocco na Tunisia zitawakilisha kanda ya kwanza barani Afrika, Nigeria na Ghana kutoka kanda ya pili, Uganda, Burundi, Kenya na Ushelisheli kutoka kanda ya Afrika Mashariki nayo Botswana, Mauritius, Namibia na Zimbabwe kutoka kanda la tano.

“ Nafasi ya kwanza na pili kutoka kila kundi zitachuana kwenye mchujo ambapo mshindi atapandishwa ngazi hadi daraja la pili nazo timu zitakazovuta mkia zitapambana kwenye mchujo wa kushuka daraja,” alisema katibu mkuu wa shirikisho la Tenisi nchini Kenya, Wanjiru Karani ambaye pia ndiye msimamizi wa mashindano hayo.

Wanjiru aliongeza kuwa umuhimu wa kuandaa mashindano hayo barani Afrika utachochea mchezo wa tenisi nchini Kenya, kuinua vipaji vya kina dada pamoja pia na kuwatia moyo wachezaji wa tenisi barani Afrika. Awali mashindano haya yaliandaliwa barani Uropa yakihusisha mataifa ya Uropa na Afrika.

“Afrika inakua sasa na tunatumai Afrika itaandaa mashindano ya Grand Slam wakati mmoja,” aliongeza Karani.

Waandalizi wa mashindano ya Billie Jean King yatakayofanyika jijini Nairobi kati ya Juni 12-17 2023.
Waandalizi wa mashindano ya Billie Jean King yatakayofanyika jijini Nairobi kati ya Juni 12-17 2023. © Tennis Kenya

Ushirikiano baina ya mataifa hayo ni mkubwa haswa kwenye mechi za ukanda mashabiki hushabikia kila timu bila ubaguzi. Tanzania imejiunga na ITF Billie Jean King Cup hivi majuzi tu. Mchezaji nambari moja barani Afrika ni mzawa wa Burundi – Saada Nahimana.

“Tunazidi kutiana moyo na mwaka jana tulikutana kama Afrika Mashariki tukakubaliana kuwa ni lazima tuandae mashindano ya kimataifa. Sasa Kenya itaandaa mashinda tisa ya chipukizi, Rwanda na Uganda zitaandaa tatu kila mmoja mwaka huu.

Burundi iliandaa moja Desemba mwaka jana. Unaona jinsi tunavyokuwa na wachezaji wetu sasa hawana tatizo la kusafiri umbali,” alisisitiza Wanjiru ambaye alishiriki makala ya Billie Jean King ya mwaka 1995 kama mchezaji akiiwakilisha Kenya. Alimaliza taaluma yake ya uchezaji kama chipukizi akiorodheshwa nafasi ya tano barani Afrika.

Maandalizi ya uwanja wa Nairobi club
Maandalizi ya uwanja wa Nairobi club © Tennis Kenya

Rais wa shirikisho la tenisi nchini Kenya James Kenani alisema kuandaa mashindano hayo kutaimarisha umaarufu wa tenisi na kuchochea ukuaji wa mchezo huo nchini Kenya. Ila alilalamikia serikali kujitenga na mchezo huo katika kutoa misaada.

“Kwa miaka miwili iliyopita, shirikisho halikupata usaidizi wowote wa kifedha kutoka kwa serikali. Serikali pia haijaanza ujenzi wa viwanja 26 vya tenisi vya umma katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Moi Kasarani licha ya ahadi iliyotolewa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2019.

Tunaiomba serikali ya sasa kupitia wizara ya michezo izingatie tenisi pia kama tu inavyozingatia soka,” alisema James Kenani.

Kikosi cha Kenya kwenye mashindano hayo, kitaongozwa na Angella Okutoyi ambaye mwaka 2022 alikuwa mkenya wa kwanza kushinda taji la Grand Slam katika mashindano ya Wimbledon akishirikiana na Rose Marie Nijkamp kutoka Uholanzi.

Kwenye mashindano ya Australian Open mwaka 2022, Okutoyi alikua mwakilishi wa kwanza wa Kenya kushinda mechi ya wasichana ya Grand Slam. Pia alishiriki mashindano ya French Open na US Open mwaka 2022 kitengo cha chipukizi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.