Pata taarifa kuu

Klabu Ya Simba Yapewa Motisha Na Mdhamini kuelekea Mechi Ya Klabu Bingwa.

NAIROBI – Nchini Tanzania, Klabu ya Simba Sports Club imepokea marupurupu ya Shilingi 100 milioni pesa yaTanzania kutoka kwa mdhamini wao mkuu, kuelekea mchezo wao wa Jumamosi wa robo fainali ya ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Club Athletic ya Morocco. 

Wachezaji wa klabu ya Simba ya nchini Tanzania
Wachezaji wa klabu ya Simba ya nchini Tanzania © simba
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa mfadhili wa klabu hiyo, nyongeza hio ni ya kuwapa motisha zaidi wanapojiandaa katika mechi yao ya robo fainali katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika. 

Vigogo hao kutoka Mtaa wa Msimbazi watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi wa michuano hiyo saa kumi jioni saa za Afrika mashariki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, jumamosi hii. 

Akizungumza jana Jumatano, Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet, Allen Mushi, amedhibitisha kuwa amemkabidhi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba Sports Club Imani Kajula fedha hizo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye hoteli ya Serena. 

Mushi alisema wanajivunia mafanikio yaliyofikiwa na klabu hiyo hadi sasa na kwamba anaamini wataendelea kung’ara katika mashindano hayo. 

Pia, alieleza kuwa fedha hizo ni sehemu ya wajibu wao wa udhamini na wataendelea kuwapa bonasi kadri wanavyoendelea kufanya vizuri. 

“Tunajivunia sana mafanikio ya klabu katika michuano ya klabu bingwa barani. Walifanya vyema katika michuano iliyopita ya Kombe la Shirikisho Afrika na safari hii wanafanya vyema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Mushi. 

Kwa upande wake, Kajula alieleza kuwa wako tayari kukabiliana na mabingwa watetezi wa shindano hilo na kuwataka mashabiki wa soka kuhudhuria pambano hilo. 

"Sisi ni klabu kubwa na tunaendelea kuifanya timu kuwa miongoni mwa bora barani," alisema Kajula. 

Katika hatua nyingine, wachezaji wa Simba wameanza kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi baada ya kupata kibarua kigumu dhidi ya wapinzani wao, Young Africans (Yanga) kwenye Ligi Kuu ya NBC na kushinda mabao 2-0. 

Ofisa Habari wa Simba Sports Club Ahmed Ally amesema kuwa wachezaji wawili Sadio Kanoute na kipa chaguo la kwanza Aishi Manula ni miongoni mwa wachezaji waliojiunga na timu hiyo baada ya kuwa majeruhi. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.