Pata taarifa kuu

Changamoto za Kinadada katika Michezo

NAIROBI – Na Paul NziokiMwezi machi umeanza kwa kasi na kama ilivyo kawaida ya dunia kuna siku kadhaa za kuadhimishwa. Tarehe mbili imekua ni siku ya wanawake duniani na vitu kadhaa vinazungumziwa ikiwemo na swala la michezo.

Harambee Starlets ya Kenya
Harambee Starlets ya Kenya © FKF
Matangazo ya kibiashara

Kuwaangazia wanawake bila ya kutaja mzizi ambao ni mtoto wa kike ni kukosa adabu kama mwandishi.

Msichana anashiriki katika michezo yote kuanzia ndondi, kriketi, mpira wa vikapu, mpira wa magongo, tenisi, soka hadi michezo ya ndani. Ila wanakoshiriki pia kuna changamoto.

Changamoto za kinadada katika michezo ni nyingi kuanzia katika Usawa wa mishahara, idadi ndogo ya watazamaji, dhulma za kingono na fursa za jumla zilizopo katika ulimwengu wa ushindani.

Hivi majuzi waendesha baiskeli wa kike katika Mashindano ya Tour de femme walilalamika wakitaka walipwe sawa na wale wa kiume kwenye Tour de france.

Mshindi katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika kwa wanawake anapewa Elfu mia nne (400 000) Dola za Marekani na mshindi wa pili anashinda Elfu mia mbili hamsini (250 000) Dola za Marekani.

Mshindi wa mashindano haya katika upande wa wanaume anashinda milioni 2.5 Dola za marekani huku mshindi wa pili akipata milioni 1.25 Dola za marekani.

Hii inaweka wazi kua kilio cha kinadada kuhusu ukosefu wa usawa katika mishahara na thamani ya mataji kinaweza kuendelea.

Kwa nini Mishahara ya Wachezaji kinadada sio sawa na ya wanaume

Sio swala ambalo lina ukakasi wa kutafuta majibu. Michezo ni biashara na katika biashara kuna uwekezaji na zao au matokeo ambayo ni faida.

Wawekezaji wengi wanaekeza katika soka la wanaume na hivyo kupata faida kubwa inayowawezesha kuwalipa wachezaji wa kiume mishahara minono.

Huu uwekezaji haupo katika michezo wanaposhiriki wanawake.

Kwa nini Uwekezaji ni mdogo kwa michezo wanayoshiriki kinadada

Wawekezaji wanaekeza katika sehemu ambayo wanaweza kupata faida kwa sababu michezo ni biashara.

Wawekezaji wanawekeza katika mchezo ambao watazamaji ni wengi na idadi ya mashabiki.

Ukiwa Tanzania gumzo ni Yanga na Simba, Rwanda Rayon sport, APR na kiyovu ni maarufu sana, Kenya Gor Mahia na Afc Leopards ndio gumzo mitaani na duniani kote tunafahamu ligi Kuu nchini England kwa wanaume inafuatiliwa sana.

Ni kwa nini sio vilabu vya kinadada? Ni kwa nini sio simba Queens na Lady Doves? Mashabiki wengi duniani wanafuata michezo wanayoshiriki wanaume.

Hii ndio hali inayowakumba wawekezaji wanaotaka kuinua kila mchezo upande wa kinadada.

Suluhu la changamoto hizi

Nitaanza na dhulma kingono ambapo naamini ni ukosefu wa nidhamu na maadili katika jamii. Kesi nyingi zimeripotiwa duniani kuhusu swala hili.

Hivi majuzi kisanga cha wasichana wa timu ya Transnzoia falcons ya nchini Kenya kilikua gumzo katika mitandao ya kijamii. Kufikia sasa vyombo vya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki havijazungumzia hatua walizopigia katika uchunguzi wao.

Utepetuvu wa vyombo vya sheria kuwapa haki wasichana waliodhulumiwa ndio kizingiti kikubwa cha kumaliza uovu huu.

Mwandishi wa Makala haya anatoa changamoto kwa vyombo vya sheria, kutafuta suluhu la haraka hili kuokoa kinadada waliodhulumiwa. Faini na adhabu kubwa zafaa pia kutolewa kwa wahusika.

Pili, swala la mishahara sawa. Binafsi sio muumini wa mishahara sawa kwa sababu naamini wapo wanawake wanaolipwa mishahara minono kuliko wanaume katika sekta nyingine.

Kila mwanamichezo alipwe kulingana na kiwango chake na mchango wake katika biashara au mchezo husika pasipo na kuangalia jinsia yake. Kando na kupata mshahara sawa, itakuaje ata kinadada wanaochezea Lyon ya ufaransa wakipata mshahara mrefu kuliko wenzao wa kiume?

Sasa ndio tuwe katika njia sawa ya kupata tunachokihitaji. Tuanze katika shule zetu. Viongozi na shule kila mahali wanapaswa kutoa ufadhili na fursa sawa kwa timu zote, iwe ni kwa vifaa, makocha au usaidizi mwingine.

Changamoto ya mwisho ni kwa watazamaji na mashabiki wanaofurika viwanjani kuangalia michezo ambayo wahusika  ni kinadada. Ni wachache ambao wanatazama na kufuatilia. Ukiwauliza mashabiki wengi wa michezo wataje wachezaji wa kike kwa majina yao utashangaa sana.

Kama jamii tunafaa kuwakumbatia wachezaji kinadada kama wachezaji wa kiume. Jamii inafaa kumwelewa akiwa uwanjani ni mchezaji na wala sio kutembea viwanjani kuwatamani kwa maumbile yao.

Wakicheza na wakishinda tuwashangilie. Vyombo vya habari tumulike wanakocheza kinadada kama ilivyo kwa wanakocheza wanaume.

Nikihitimisha Makala haya, Michezo ni ajira na afya na kinadada wana haki ya kupata vyote.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.