Pata taarifa kuu
UCHAMBUZI

Kwanini Messi hatostaafu hivi karibuni licha ya kushinda kombe la dunia

Lionel Andres Messi hatimaye, baada ya mahangaiko na magumu mengi katika taaluma yake ya soka amefanikiwa kupata kombe pekee ambalo lilikua linakosekana katika kabati lake binafsi la vikombe. Messi alishinda Copa America mwaka 2021 miogoni mwa mataji mengine.

Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionell Messi
Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionell Messi AP - Martin Meissner
Matangazo ya kibiashara

Kwenye makala ya Kombe la Dunia 2014, Messi alitajwa mchezaji bora wa mashindano akiwa na umri wa miaka 27, Argentina ilipoteza 1-0 kwenye fainali dhidi ya Ujerumani. Miaka miwili baadaye, Messi alistaafu soka baada ya kuonekana  kukata tamaa baada ya kupoteza fainali nne akiwa na timu ya taifa.

Mashabiki wengi nchini Argentina walimsuta sana wakidai, Messi alionesha viwango bora akiwa Barcelona tofauti sana na akiwa timu ya taifa. Safari hii mwaka 2022, Messi ameishindia Argentina taji la tatu la dunia akitajwa mchezaji bora tena. Hakika sasa atakubalika kama alivyokubalika Diego Armando Maradona.

Lionell Messi, akiwaongoza wachezaji wenzake kusherehekea ushindi wa kombe la dunia, Desemba 18 2022 nchini Qatar
Lionell Messi, akiwaongoza wachezaji wenzake kusherehekea ushindi wa kombe la dunia, Desemba 18 2022 nchini Qatar AP - Martin Meissner

Nafikiri kwa sasa ule mjadala mrefu wa nani mchezaji bora katika historia ya soka, umepata jibu. Ronaldo na Messi wameonyesha viwango bora kila mmoja akielekea Qatar kusaka taji la dunia ambalo lingesuluhisha huu mjadala.

Tukizingatia mataji au mafanikio uwanjani basi nafikiri Messi huna budi ila kukubali ndiye mchezaji bora wa nyakati zote, maarufu kama G.O.A.T

Kabla ya Kombe la Dunia kuanza, Leo Messi alitangaza kuwa haya ndio Makala yake ya mwisho kucheza na pia kabla ya fainali alisema kuwa fainali utakua mchezo wake wa mwisho akivalia jezi ya La Albiceleste.

Ila kinyume na ahadi zake, deni hilo inaonekana atailipa baadaye wala si sasa. Baada ya kuishinda Ufaransa kwenye fainali, Messi alitangaza kuwa bado ataendelea kuchezea Argentina. Kwa nini ahisi hivi ?

Mchezaji wa zamani wa Uingereza, Michael Owen amewahi kusema, “Mchezaji hubaini wakati wa kustaafu pale ambapo anachukizwa na swala la kuamka asubuhi kuenda mazoezini.”

Timu ya taifa ya Argentina, ilipowasili katika jiji la Bueno Aires na kulakiwa na mamilioni ya mashabiki wa nchi hiyo, Desemba 20  2022
Timu ya taifa ya Argentina, ilipowasili katika jiji la Bueno Aires na kulakiwa na mamilioni ya mashabiki wa nchi hiyo, Desemba 20 2022 REUTERS - MARTIN VILLAR

Tangu Messi aanze kuichezea Argentina mwaka 2005, amepokea vijembe vingi sana na safari yake kwenye timu ya taifa imekua ngumu zaidi. Alifika kwenye fainali nne na kupoteza zote Copa America 2007, 2015 na 2016, Kombe la Dunia 2014 kisha kumaliza nafasi ya tatu kwenye Copa America 2019.

Unaambiwa usikate tamaa kamwe. Mwaka 2021, Messi hatimaye alishinda kombe la Copa America baada ya kuishinda Brazil kwenye fainali. Baada ya hapo ikabakia mtihani mmoja tu akamilishe malengo. Kombe la dunia 2022.

Nyama ya kichwa ni tamu, ila ya mkia ni tamu pia. Wengi watasema Messi anastahili kustaafu akiwa na rekodi hii nzuri, asirudi kucheza mambo yakwende mrama ndipo astaafu. Heri aondoke kichwa chake na sifa yake ikiwa juu. Lakini nahisi tofauti.

 

Nahodha wa Argentina  Lionel Messi
Nahodha wa Argentina Lionel Messi REUTERS - KAI PFAFFENBACH

Ndani ya miaka 17, Messi alicheza chini ya kivuli cha Maradona bila kujihisi bingwa. Naamini sasa anataka kuendelea kucheza ili angalau anapoingia uwanjani ahisi jinsi kina Maradona, Pele, Johan Cruyff, Alfredo Di Stefano, George Best walivyokuwa wanahisi wanapocheza kibingwa.

Kwake Messi, haijalishi ikiwa mambo yataenda vibaya ila muhimu zaidi ni kuvaa jezi ya Argentina kama bingwa tofauti na zamani alipokuwa akicheza kama jogoo anayejifunza kuwika. Sasa ana ufahamu na sauti nzuri ya kuwika asubuhi majogoo.

Mimi husema kama asali inaua, sumu ya kazi gani? Nuka vumbi mchana, usiku fukiza udi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.