Pata taarifa kuu
AFCON 2017

Cameroon walivyoshinda taji la AFCON 2017

Cameroon ndio mabingwa wapya wa soka baina ya mataifa ya bara Afrika.

Mabingwa wa taji la AFCON mwaka 2017
Mabingwa wa taji la AFCON mwaka 2017 RFI/Pierre René-Worms
Matangazo ya kibiashara

Hii ilikuja mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kuifunga Misri mabao 2-1 katika fainali ya makala ya 31 ya michuano ya AFCON mwaka 2017  iliyomalizika katika uwanja wa l'Amitie jijini Libreville nchini Gabon.

Cameroon ilitoka nyuma na kupata ushindi huo muhimu ambao sasa umewapa ufalme wa soka barani Afrika na kuwapa rekodi ya kunyakua taji hili kwa mara ya kwanza baada ya kulisubiri miaka 15.

Ni ushindi ambao umeifanya Cameroon kuweka historia ya kushinda taji hili sasa mara tano mwaka 1984, 1988, 2000, 2002 na 2017.

Misri ilianza vema mchuano huo wa fainali baada ya kupata bao la mapema kupitia mshambuluaji wake Mohamed Elneny katika dakika ya 22 ya mchuano huo.

Hata hivyo, furaha ya Misri haikudumu muda mrefu baada ya Nicolas Nkoulou, kuisawazishia Cameroon katika dakika ya 59 ya kufanya timu zote kutoshana nguvu katika kipindi cha pili.

Juhudi za Misri kupenya na kupata bao katika ngome ya Cameroon zilishindikana na kuacha mambo kuendelea kuwa sare kuelekea katika dakika za lala salama za mchuano huo.

Dakika mbili kabla ya kukamilika kwa muda wa kawaida, Cameroon kupitia mchezaji wake Vincent Aboubakar, aliwanyanyua mashabiki wa nchi yake kwa kufunga bao la ushindi katika dakika 88 na kuwamaliza nguvu mashabiki na wachezaji wa Misri.

Refarii kutoka Zambia Janny Sikazwe alipopuliza kipenga cha mwisho, ilikuwa ni furaha kubwa kwa wachezaji na mashabiki wa Cameroon waliofurika uwanjani baada ya kubaini kuwa wao ni mabingwa.

Ushindi huu wa Cameroon umekuwa kama wa kulipiza kisasi cha mwaka 2008, wakati Misri ilipoishinda kwa bao 1-0 nchini Ghana.

Mashabiki wa Cameroon barani Afrika na hasa jijini Yaounde wameendelea kusherehekea ushindi huu wakisubiri kikosi cha taifa kurejea nyumbani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.