Julius Yego amaliza wa pili katika mchezo wa urushaji mkuki
Mkenya Julius Yego ameshinda medali ya fedha katika mchezo wa kurusha mkuki katika Michezo ya Olimpiki nchini Brazil.
Imechapishwa:
Yego ambaye ni bingwa wa dunia, na anashikilia rekodi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, katika Michezo hii ya Olimpiki alirusha kwa umbali wa Mita 88.24.
Wakati wa kuelekea kwenye Michezo hii, Yego mwenye umri wa miaka 27, alikosa tiketi ya kwenda Brazil katika uwanja wa ndege jijini Nairobi na kuzua hali ya wasiwasi.
Yego aliyefahamika kwa jina la utani kama 'YouTube man' anaendelea kukumbukwa, kwa kujifunza mchezo huu wa kurusha mkuki kupitia mtandao wa Yutube na baadaye kuwa bingwa wa dunia.
Nafasi ya kwanza katika mchezo huu, ilichukuliwa na Thomas Rohler aliyerusha umbali wa Mita 90 nukta 30 na kuipa ushindi nchi yake ya Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu Michezo ya mwaka 1972 mjini Munich.
Keshorn Walcott kutoka Trinidad & Tobago akimaliza wa tatu na kuipa nchi yake medali ya shaba kwa kurusha umbali wa Mita 85 nukta 38.