Pata taarifa kuu
FIFA-SOKA-BLATTER

Mwanamfalme wa Jordan atangaza nia kuwania kiti cha urais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani, fifa

Makamu wa rais wa shirikisho la kabumbu duniani, FIFA, mwana mfalme Ali Bin Al Hussein ametangaza rasmi nia yake ya kuwania nafasi ya kuongoza shirikisho hilo kupambana na rais wa sasa Sepp Blatter. 

Makamu wa rais wa Fifa, Ali Bin Al Hussein (Kushoto) akiwa na rais wa Fifa, Sepp Blatter (Kulia) wote wanawania nafasi ya kuongoza shirikisho hilo
Makamu wa rais wa Fifa, Ali Bin Al Hussein (Kushoto) akiwa na rais wa Fifa, Sepp Blatter (Kulia) wote wanawania nafasi ya kuongoza shirikisho hilo Fifa online
Matangazo ya kibiashara

Mwanamfalme huyo wa Jordan anakuwa mgombea wa pili kutangaza nia yake ya kupambana na Blatter kwenye uchaguzi ujao, uchaguzi ambao Blatter anatarajiwa kuwania nafasi hiyo kwa muhula wa tano.

Akizungumza baada ya kutangaza uamuzi wao, Ali amesema kuwa umefika wakati wa kuhamisha mijadala kuhusu fifa na kuleta mijadala muhimu kuhusu masuala ya michezo.

Ali ameongeza kuwa “Vichwa vya habari vinapaswa kuhusu mpira wa miguu na sio kuhusu fifa”. Alisema mwanamfalme huyo wa Jordan.

Rais wa Fifa, Sepp Blatter (Kushoto) akiwa na rais wa Uefa, Mitchel Platin (kulia)
Rais wa Fifa, Sepp Blatter (Kushoto) akiwa na rais wa Uefa, Mitchel Platin (kulia) © AFP

Mwanamfalme Ali akaongeza kuwa “mchezo wa dunia unahitaji kuwa na shirikisho makini, taasisi ambayo ni msaada wa mashirikisho mengine na yenye kufuata maadili, uwazi na utawala bora”.

Uamuzi wa Ali umeonekana kumfurahisha rais wa shirikisho la mpira barani Ulaya UEFA, Mitchel Platin ambaye ameahidi kuhakikisha anamsaidia kupata kura nyingi iwezekanavyo kwenye uchaguzi toka mashirikisho ya Ulaya.

Mwezi mmoja uliopita nahodha wa zamani wa Uingereza Gary Lineker alilifananisha shirikisho la mpira wa miguu duniani fifa kama taasisi isiyo na maadili kufuatia taasisi hiyo kutuhumiwa kwa rushwa.

Balozi wa zamani wa shirikisho hilo, Jerome Champagne ambaye alijiunga na shirikisho hilo mwaka 1999, ndiye mgombea pekee ambaye ametangaza wazi kuwa atawania kiti cha urais kwenye shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa kelenda ya uchaguzi ya Fifa, wagombea wenye nia ya kuwania nafasi ya urais wanapaswa kuwa wametangaza nia mpaka kufikia tarehe 29 ya mwezi January mwaka huu.

Sepp Blatter anaingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu akiwa na imani kubwa ya kujizolea kura nyingi toka kwa wajumbe wa bara la Afrika ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakimuunga mkono.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.