Pata taarifa kuu
UINGEREZA-SOKA

Manchester United yakanusha uvumi uliozagaa ya kwamba Wayne Rooney atauzwa mwishoni mwa msimu huu

Klabu ya Manchester United imepuuzilia mbali uvumi uliozagaa ya kwamba Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uingereza anayekipiga katika timu hiyo Wayne Rooney atauzwa mwishoni mwa msimu huu. Manchester United imekanusha uvumi huo kupitia Msemaji wa Klabu hiyo umesema hakuna mpango wowote wa kuuzwa kwa Mshambuliaji huyo aliyetumikia timu hiyo kwa miaka tisa sasa.

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney akishangilia goli alilofunga dhidi ya Liverpool
Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney akishangilia goli alilofunga dhidi ya Liverpool Shaun Botterill/Getty Images
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Manchester United amesisitiza Rooney mwenye umri wa miaka 27 ataendelea kuwepo katika klabu hiyo na hawezi kuondoka eti kwa kuwa Kocha Mkuu Sir Alex Ferguson ametangaza kustaafu mwishoni mwa msimu huu.

Tamko la Manchester United limekujwa baada ya kuwepo taarifa Rooney ameomba kuondoka kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu sasa taarifa ambazo zimetajwa kuwa ni uzushi mtupu.

Taarifa hizi zinakuja na kuongezewa nguvu ya kwamba Rooney alishamuomba Sir Ferguson kuondoka Manchester United kipindi cha majuma mawili yaliyopita lakini ombi lililokataliwa na Kocha huyo.

Rooney anatajwa kuwa aliomba kuondoka Manchester United na kumueleza Sir Ferguson ya kwamba huu ni wakati wake muafaka kuondoka baada ya kuitumikia Klabu hiyo kwa kipindi cha miaka tisa akitokea Everton.

Uvumi wa kuondoka kwa Rooney unakuja ikiwa ni siku moja baada ya Sir Ferguson kutangaza kustaafu wadhifa wake na wengi walianza kutoa taarifa hizo punde tu baada ya mchezaji huyo kuonekana akikosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Mshambuliaji huyo anaelezwa alikuwa na hasira baada ya kuwekwa benchi katika mchezo dhidi ya Real Madrid ambapo Danny Welbeck alianza kwenye mchezo huo ambao Manchester United haikufanya vizuri.

Rooney msimu huu amekuwa akibadilishwa mara kadhaa tangu Manchester United imsajili Robin Van Persie ambaye alipewa jukumu la kuwa mshambuliaji kinara na kuweza kuisaidia kutwaa taji la 20.

Tangu Rooney ajiunge na Manchester United mwezi Agosti mwaka 2004 amecheza michezo 402 na kufunga magoli 197 huku msimu huu akifunga magoli 16 katika michezo 37 aliyoshuka dimbani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.