Pata taarifa kuu
EUROPA-UINGEREZA-UTURUKI-URENO

Chelsea, Benfica zatamba Europa huku Newcastle, Rubin Kazan na Tottenham mambo yakiwaendea kombo

Mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Mashindano ya UEROPA umeendelea jana na kushuhudia michezo minne ikipigwa na miamba nane kuchunua kusaka nafasi nne za kutinga hatua ya Nusu Fainali. Chelsea wakiwa nyumbani Stamford Bridge wamefanikiwa kuchomoza na ushindi mnono wa magoli 3-1 dhidi ya Rubin Kazan na kujiwekea mazingira mazuri ya kutinga hatua ya Nusu Fainaliya Mashindano hayo.

Mshambuliaji wa Chelsea Fernando Torres akifunga goli la pili dhidi ya Rubin Kazan
Mshambuliaji wa Chelsea Fernando Torres akifunga goli la pili dhidi ya Rubin Kazan
Matangazo ya kibiashara

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uhispania Fernando Torres alionesha makali yake baada ya kufanikiwa kuzifumania nyavu za wapinzani wake mara mbili na kurejesha matumaini kwa mashabiki wake.

Victor Moses raia wa Nigeria yeye alifunga goli la pili huku Rubin Kazan wakipata goli lao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti baada ya John Terry kushika mpira na Bibras Natkho akaweka mpira kimiani.

Mchezo mwingine ulishuhudia Newcastle United wakiambulia kichapo cha magoli 3-1 wakiwa ugenini kukabiliana na Benfica ya Ureno iliyoweza kuutumia vyema kabisa uwanja wake wa nyumbani wa Estadio da Luz.

Newcastle inayonolewa na Alan Pardew ilikuwa ya kwanza kupata goli kupitia kwa Papiss Cisse kabla ya Benfica hawajazinduka na kulishambulia kwa nguvu lango la wapinzani wake kupitia Rodrigo Moreno akasawazisha goli hilo.

Benfica wakazidi kuliandama goli la wapinzani wao na ndipo Rodrigo Jose Lima akafanikiwa kufunga goli la pili kabla ya Oscar Cardozo kufunga goli la tatu kwa mkwaju wa penalti.

Licha ya Newcastle kupata kichapo hicho lakini Mshambuliaji wake Cisse alikosa nafasi nyingi za wazi huku michomo yake miwili ikigonga mwamba na Moussa Sissoko akionekana kung'aa vilivyo.

Mchezo mwingine ulishuhudia vijana wa Fenerbahce wakiibuka na ushindi wa jioni wa magoli 2-0 dhidi ya wachezaji kumi wa Lazio na kujiweka sawa kabla ya mchezo wa marudiano juma lijalo.

Pierre Webo alikuwa wa kwanza kuweka mpira kimiani kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Lazio Stefan Radu kunawa mpira kwenye eneo la hatari na hivyo mwamuzi kuamua ipigwe penalti.

Lazio walilazimika kumaliza wakiwa na wachezaji kumi uwanjani baada ya Ogenyi Onazi kulimwa kadi ya pili ya njano na hivyo kutolewa nje na ndipo Mshambuliaji Dirk Kuyt akafunga goli la pili.

Tottenham wakiwa nyumbani wenyewe walijikuta wanabanwa mbavu na wageni wao Basel FC baada ya kulazimishwa sare ya magoli 2-2 huku pia wakimpoteza Mshambuliaji wao Gareth Bale aliyepata maumivu ya kiwiko cha mguu.

Basel ilikuwa ya kwanza kupata goli kupitia Valentin Stocker aliyeachia mkwaju mkali kabla ya Fabian Frei kufunga goli la pili na kuonesha njia ya Tottenham kutinga Nusu Fainali imejawa na magugu.

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Togo Emmanuel Adebayor alifanikiwa kurejesha goli moja kabla ya dakika arobiani na tano za kwanza hazijamalizika na kufanya matokeo kuwa magoli 2-1.

Kipindi cha pili wachezaji wa Tottenham waliendelea kupigana kufa na kupona kuhakikisha wanasawazisha goli hilo na hata kupata ushindi na ndipo Gylfi Sigurdsson akafanikiwa kufunga goli la pili kwa upande wao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.