Pata taarifa kuu

Emmanuel Macron atangaza kutumwa kwa meli ya kijeshi 'kusaidia' hospitali Gaza

Mara tu baada ya kutangazwa, meli ya Ufaransa inayotoa huduma za matibabu, Tonnerre, imeanza safari siku ya Jumatano, Oktoba 25, kuelekea Gaza, ambako itashiriki katika shughuli za kutoa msaada kwa raia.

Emmanuel Macron na Abdel Fatah al-Sissi mjini Cairo, Oktoba 25, 2023.
Emmanuel Macron na Abdel Fatah al-Sissi mjini Cairo, Oktoba 25, 2023. AP - Christophe Ena
Matangazo ya kibiashara

Baada ya Israel, Ukingo wa Magharibi na Jordan, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaendelea na ziara yake ya Mashariki ya Kati na kwa sasa yuko mjini Cairo. Wiki mbili na nusu baada ya shambulio la Hamas nchini Israel na kuanza kwa mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza kama ulipizaji kisasi, rais wa Ufaransa ametaka kukanusha shutuma zilizotolewa na viongozi mbalimbali dhidi ya nchi za Magharibi, kwamba "maisha ya Wapalestina hayana thamani sawa na maisha ya Waisraeli." "Ufaransa inawachukulia watu wote sawa. Sheria ya kimataifa inatumika kwa kila mtu na Ufaransa daima imekuwa ikizingatia maadili ya ulimwengu ya ubinadamu (...) Waathiriwa wote wanastahili huruma yetu, ahadi yetu kwa ajili ya amani ya kweli na ya kudumu katika Mashariki ya Kati," Emmanuel Macron amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Abdel Fatah Al-Sisi.

Ili kuunga mkono kauli zake, rais wa Ufaransa ametangaza kuwasili siku ya Alhamisi mjini Cairo ndege iliyobeba vifaa vya matibabu vya dharura, pamoja na meli ya kikosi cha wanamaji kuondoka huko Toulon "katika saa 48 zijazo" kuelekea Gaza "kusaidia hospitali" ambazo zinakabiliwa na uhaba wa dawa na kwa baadhi ukosefu wa umeme. Tangazo hilo limeanza kutekelezwa mara moja: Shirika la habari la AFP linaripoti kwamba meli ya Ufaransa, Tonnerre, inayotoa huduma za matibabu, imeanza safari kuelekea Gaza. Meli hiyo iliondoka kwenye bandari ya Toulon "ili kuimarisha mfumo wetu mashariki mwa Mediterania, ambapo itaungana na meli za Alsace na Surcouf," msemaji wa Jeshi la Wanamaji la Ufaransa amesema.

Emmanuel Macron pia amezindua ombi jipya la kuunga mkono suluhu la kisiasa la mzozo huu, likihusisha, kwa mujibu wake, kuanzishwa upya kwa mchakato wa amani kwa lengo la kufanikisha kuundwa kwa taifa la Palestina na kuhalalisha uhusiano kati ya Israel na nchi za Kiarabu. "Lazima tuchukue hatua madhubuti leo ili hatimaye kufikia suluhu la Serikali mbili, huku Israel na Palestina zikiishi bega kwa bega kwa amani na usalama," amesema mkuu wa nchi, ambaye mwenzake wa Misri alimshukuru kwa moyo mkunjufu kwa mpango wake huo.

"Sio kwa sababu wazo hili ni la zamani ndio limepitwa na wakati (...) Njia hii ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inatoa nafasi nzuri, ambayo sio ya vurugu, ambayo ni utambuzi wa haki halali, ambayo kutoa mfumo, ule wa mijadala ya kisiasa. Ni lazima tufanye hivyo,” amesisitiza Emmanuel Macron.

(Pamoja na mashirika)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.