Pata taarifa kuu
USHIRIKIANO-DIPLOMASIA

Iran na Saudi Arabia zakubali kurejesha uhusiano wa kidiplomasia

Iran na Saudi Arabia zimekubali kurejesha uhusiano wa kidiplomasia, chombo cha habari chenye uhusiano na serikali ya Iran kimeripoti Ijumaa, Machi 10, kikinukuu taarifa ya pamoja kutoka kwa nchi hizi mbili zenye nguvu za Mashariki ya Kati ambazo uhusiano wao ulikuwa umevunjika tangu mwaka 2016.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran Ali Shamkhani, kulia akipeana mkono na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi, wakati mshauri wa usalama wa taifa wa Saudia Musaad bin Mohammed al-Aiban akitazama wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano kati ya Iran na Saudi Arabia mjini Beijing, Ijumaa hii. Machi 10, 2023.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran Ali Shamkhani, kulia akipeana mkono na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi, wakati mshauri wa usalama wa taifa wa Saudia Musaad bin Mohammed al-Aiban akitazama wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano kati ya Iran na Saudi Arabia mjini Beijing, Ijumaa hii. Machi 10, 2023. AP
Matangazo ya kibiashara

"Baada ya mazungumzo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ufalme wa Saudi Arabia wamekubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi na uwakilishi (wa kidiplomasia) ndani ya kipindi cha miezi miwili," imesema taarifa hiyo, limebaini shirika la habari la Irna, likinukuu taarifa hiyo, ambayo pia imetolewa na shirika la habari la serikali la Saudia SPA.

Saudi Arabia, nchini yenye wakaazi wengi wa madhehebu ya Kisunni na Iran yenye wakaazi wengi wa madhehebu ya Kishia zilivunja uhusiano miaka saba iliyopita baada ya waandamanaji katika Jamhuri ya Kiislamu kushambulia ofisi za kidiplomasia za Saudia kufuatia hukumu ya Riyadh ya kumuua kiongozi mashuhuri wa Kishia, Nimr al-Nimr.

Kwa mujibu wa Irna, Ali Shamkhani, katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa, alisafiri hadi Beijing, nchini China, siku ya Jumatatu 'kwa mazungumzo ya kina na mwenzake wa Saudia, yenye lengo la kusuluhisha tofauti kati ya Tehran na Riyadh'.

Tangu mwezi Aprili 2021, Iraq imekuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa kati ya maafisa wa usalama kutoka mataifa hayo mawili hasimu ili kuzileta pamoja nchi hizo mbili.

Katika taarifa yao ya pamoja, Iran na Saudi Arabia “zinaishukuru Jamhuri ya Iraq na nchi ya Oman kwa kuandaa mazungumzo kati ya pande hizo mbili mwaka 2021 na 2022, pamoja na viongozi na serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuwa mwenyeji na kuunga mkono mazungumzo katika nchi hiyo".

Tehran na Riyadh zinaunga mkono pande zinazohasimiana katika mizozo kadhaa katika ukanda huo, hasa nchini Yemen. Iran ina ushawishi mkubwa nchini Iraq na Lebanon na inaunga mkono kijeshi na kisiasa utawala wa Syria.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.