Pata taarifa kuu

Matetemeko ya ardhi: Jumuiya ya kimataifa yahimizwa kusaidia maeneo ya waasi

Waokoaji kutoka maeneo ya waasi nchini Syria wameiomba jumuiya ya kimataifa kutuma timu kuwasaidia, katika mbio za kupambana na wakati ili kuokoa watu waliokwama chini ya vifusi baada ya tetemeko kubwa la ardhi.

Watu wengi wamekwama katika vifusi vya majengo huko Diyarbakir, Uturuki, Februari 8, 2023.
Watu wengi wamekwama katika vifusi vya majengo huko Diyarbakir, Uturuki, Februari 8, 2023. © Sertac Kayar Reuters
Matangazo ya kibiashara

Idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi lililoikumba Uturuki na Syria siku ya Jumatatu imepita 11,000, wakiwemo zaidi ya 2,600 nchini Syria, nusu yao wakiwa katika maeneo ya kaskazini na kaskazini magharibi chini ya udhibiti wa waasi.

Mikoa hii iliyo karibu na Uturuki inanyimwa msaada wa serikali ya Syria na kwa kawaida hutegemea msaada kutoka Ankara, ambayo kwa sasa imekumbwa na maafa kwenye ardhi yake.

"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua majukumu yake kuhusiana na waathiriwa wa kiraia. Timu za kimataifa za uokoaji zinapaswa kuingilia kati katika maeneo yetu," msemaji wa kikosi cha White Helmets Mohammad Al - Chebli amesema.

"Ni mbio za kweli dhidi ya wakati, watu wanakufa kila sekunde chini ya vifusi," ameongeza. "Mamia ya familia bado hawajapatikana au wamenasa kwenye vifusi."

Zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 3,300 wa kikosi hiki wamehamasishwa tangu tetemeko la ardhi, lakini bado wanakosa wafanyakazi na vifaa. "Hawana mbwa wa upekuzi ili kubaini ni majengo yapi yaliyoporomoka kuna waathiriwa", aeleza Bw. Chebli.

Wakifanya kazi katika mazingira magumu, kwenye baridi na mwanga wa tochi usiku, waokoaji hao mara nyingi husaidiwa na wakazi, ambao hujaribu kuondoa vifusi kwa kutumia pikipiki au jembe na wakati mwingine mikono mitupu.

Kadiri muda unavyosonga, "nafasi ya kuokoa watu inapungua," amesema msemaji huyo, aliyehojiwa kwa simu na shirika la habari la AFP nchini Uturuki. "Tunahitaji vifaa vizito, vipuri vya vifaa vyetu."

"Timu zote zimechoka, lakini tunaendelea kufanya kazi. Kila wakati tunapofanikiwa kupata watu walio hai kutoka chini ya vifusi, inatupa nguvu na matumaini," mfanyakazi wa kujitolea ameliambia shirika la habari la AFP.

Video ambayo imesambaa mitandaoni inaonyesha umati ukilipuka kwa shangwe huku waokoaji wakiwatoa watoto wawili kutoka kwenye vifusi. "Furaha ya waokoaji ilikuwa isiyoelezeka", anasema mfanyakazi huyu wa kujitolea aliyehojiwa kutoka Sarmada katika mkoa wa Aleppo.

White Helmets hupokea ufadhili wa kigeni, na Uingereza ilitangaza Jumanne kwamba itawapa msaada wa ziada wa karibu euro 900,000. Misri, kwa upande wake, ilituma timu ya ufundi na madaktari.

Zaidi ya watu milioni nne wanaishi katika maeneo ya waasi kaskazini mwa Uturuki, karibu na Uturuki. Misaada inaletwa huko kupitia kivuko kimoja kutoka Uturuki, lakini barabara inayoelekea kwenye kivuko kutoka huko imeharibika, na kutatiza shughuli za misaada kwa muda, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Eneo la Idleb, ambako karibu watu milioni tatu wanaishi, linadhibitiwa na kundi la wanajihadi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS). Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Idlib siku ya Jumatano, afisa wa sekta ya afya ya eneo hili, Hussein Bazar, amebainisha kwamba "eneo hilo linahitaji haraka aina zote za msaada wa matibabu".

"Hali ya Idleb na maeneo yaliyokombolewa ni janga na hatuna uwezo tena wa kutoa msaada wa afya kwa watu wanaohitaji," amesema.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.