Pata taarifa kuu
UTURUKI/SYRIA - TETEMEKO LA ARDHI

Uturuki: Erdogan atangaza hali ya hatari ya miezi mitatu, maafa yakiongezeka

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na tetemeko kubwa la ardhi nchini Uturuki na Syria, imeongezeka na kufikia zaidi ya Elfu tano, wakati huu maafisa wanapoendelea na juhudi za kuwatafuta watu ambao hawajapatikana.

Shughuli ya uokoaji ikiendelea baada ya tetemeko la ardhi la Uturuki
Shughuli ya uokoaji ikiendelea baada ya tetemeko la ardhi la Uturuki AP - Omar Sanadiki
Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema nchini Uturuki pekee, watu zaidi ya Elfu tatu na mia 4 wamepoteza maisha huku huko Syria, idadi hio ikiwa zaidi ya Elfu moja na mia sita.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza hali ya hatari ya miezi mitatu katika mikoa 10 iliyoathirika, akisema mikakati zaidi ya dharura itachukuliwa.

Tumeamua kutangaza hali ya hatari ili kuhakikisha kazi yetu ya uokoaji inafanyika haraka. Amesema Erdogan.

Nalo Shirika la afya duniani, WHO, linasema tetemeko hilo lenye ukubwa wa Ritcha 7.8, lililotokea wakati watu wakiwa wamelala Jumatatu na kusababisha majengo kuporomoka, litawaathiri zaidi ya watu Milioni 23 katika nchi hizo mbili.

Ondoa vikwazo

Shirika la msalaba mwekundu nchini Syria siku ya Jumanne, limetoa wito kwa mataifa ya magharibi, kuondoa vikwazo vilivyopo dhidi ya nchi hiyo, na kutoa msaada, ili kuwafaidi raia ambao wameathirika na tetemeko la ardhi, ambapo zaidi ya raia 1,600 wamefariki katika taifa hilo lenye usalama mdogo.

Shirika hilo chini ya uongozi wa Khaled Haboubati, pia limetuma raia elfu tatu wa kujitolea ili kutoa msaada kwa waathiriwa.

Muda umefika baada ya tetemeko hili la ardhi…na naliomba shirika la umoja wa mataifa la maendeleo ya kimataifa USAID, kutoa msaada kwa raia wa Syria. Amesema Haboubati

Uchumi wa Syria umekuwa ukiyumba na kuifanya nchi hiyo kuwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na majanga makubwa, na mara kwa mara utawala wa Damascus umelaumu matatizo yake ya kifedha kwa vikwazo vya Magharibi vilivyowekwa kutokana na mzozo wa 2011 ambao ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mara ya mwisho kwa Uturuki kushuhudia tetemeko kubwa kama hili, ilikuwa ni mwaka 1939, wakati zaidi ya watu Elfu 33 walipopoteza maisha katika mkoa wa Erzincan na watu wengine Elfu 17 miaka kadhaa iliyopita katika mkoa wa Duzce.

 

  

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.