Pata taarifa kuu
KENYA-CORONA-UTALII-UCHUMI

Utalii waanza kuimarika baada ya Kenya kufungua anga lake

Baada ya serikali ya Kenya kufungua anga lake na kuruhusu kuwasili kwa wageni nchini humo kuanzia Agosti 1 na baada ya kuanza kupungua kwa maambukizi ya Corona, vivutio vya watalii vilivyokuwa vimefungwa mjini Mombasa sasa vimeanza kufunguliwa.

Makavazi ya kitaifa ya fort jesus nchini Kenya
Makavazi ya kitaifa ya fort jesus nchini Kenya Joseph Jira/RFI
Matangazo ya kibiashara

Mojawapo ya vivutio hivyo ambavyo sasa vimefunguliwa ni makavazi ya kitaifa  na ya kihistoria ya Fort jesus yanayotambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utanaduni, UNESCO.

 

Msimamizi mkuu wa makavazi hayo Fatma Twahir anasema sekta ya utalii ilipoteza mamilioni ya fedha na kufunguliwa tena kunatoa matumaini, huku akibaini kwamba kanuni za kiafya zimezingatiwa kuzuia maambukizi ya Corona.

"Tumepata idhni ya kufungua tulipata maagizo kutoka wizara ya afya viongozi sote tukapimwa COVID-19, sote bahati nzuri hatukupatikana na virusi vya Corona; Kwa hiyo tumefungua na kupokea wageni wetu wa kwanza, kuna maeneo ya kunawa mikono, na unakaa umbali wa mita 1.5, " amesema Fatma Twahir.

Wafanyakazi wengi walioathirika na hatua ya kufungwa kwa eneo hilo kama Azgal Thurab ambaye pia ni mwelekezi wa watalii eneo hilo, ana matumaini ya kunufaika kimaisha.

“Tangu ugonjwa wa COVID-19 uzuke na Fort Jesus kufungwa, maisha yamezidi kuwa magumu na kuzorota, tunatarajia wageni baada ya mwezi huu na mwezi unaokuja watakuwa ni wengi sana, ” Azgal Thurab amesema.

Jacob Kimani, mmoja wa watalii wa ndani waliosafiri kutoka jijini Nairobi, amekuwa miongoni mwa watalii wa kwanza kuzuru eneo hili la Fort Jesus, amepongeza hatua ya serikali ya kufungua anga lake.

Kwa sasa shughuli mbalimbali zinaonekana kuanza kurejea katika eneo hili lenye kivutio cha watalii nchini Kenya na wadau wana matumaini kuwa sekta hiyo imeanza kuimarika baada ya visa vya Corona kuanza kupungua na kuanza tena kwa safari za kimataifa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.