Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA

TPSF: Wafanyabishara kutoka nchi wanachama za EAC wajiamini kushindana kimataifa

Viongozi kutoka sekta binafsi nchini Tanzania wamesema pamoja na Serikali mpya ya nchi hiyo kusisitiza kuwa mazingira ya uwekezaji yako huru, bado kuna changamoto ambazo ni wazi zinaikwamisha sekta binafsi na wawekezaji wa kigeni.

Mwenyekiti wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania Reginald Mengi (aliyekaa kutoka kushoto) akiongea wakati wa mkutano wa kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania. April 6, 2017.
Mwenyekiti wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania Reginald Mengi (aliyekaa kutoka kushoto) akiongea wakati wa mkutano wa kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania. April 6, 2017. Emmanuel Makundi/RFIKIswahili
Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania Dr Reginald Mengi, amesema nchi ya Tanzania inayo rasilimali za kutosha ambazo ikiwa zingefanyiwa uwekezaji na utaratibu mzuri pengine nchi ya Tanzania ingekuwa iko mbali kwa maendeleo.

Mengi amesema mbali na changamoto zilizoko Serikalini hasa kwenye ushirikishwaji wa sekta binafsi na kutoa fursa kwa wazawa, bado nchi ya Tanzania haifanyi biashara kwa wingi na mataifa ya kigeni jambo ambalo kwa biashara amesema sio zuri sana.

Mwenyekiti huyo wa TPSF ameongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa sana kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali, makampuni ya kigeni na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kubadilishana mawazo na ujuzi wa namna bora zaidi ya kukuza uchumi kwenye taifa kama Tanzania.

Mengi amesema ikiwa ushirikiano huo utakosekana itakuwa vigumu sana kwa nchi pamoja na watu wa sekta binafsi kujua namna bora wanayoweza kushirikiana na kwamba kwa dunia ya sasa inayokua kwa kasi kwa teknolojia na ujuzi, ushirikiano baina ya wadau ni muhimu.

Dr Mengi amesema tatizo kubwa analoliona kwa wafanyabiashara wazawa ni kutojiamini hali ambayo inawafanya wengi kuhisi kuwa hawana uwezo wa kufanya biashara na makampuni ya nje.

“Tatizo watanzania wengi hawajiamini, usisubiri upate pesa ndio uone unaweza kufanya biashara, pesa isiwe sababu ya wewe kushindwa kufanya biashara kimataifa.” alisema Mengi.

“Lazima tujijengee uwezo na tujiamini kuwa tunaweza tusisubiri kupewa misaada kila wakati, hata leo ukijaribu unaweza kufika mbali. Mimi binafsi nilizaliwa kwenye nyumba ya udongo, lakini umasikini tuliokuwa nao haukunifanya nikate tamaa na leo hii niko hapa na najiona ni mtu muhimu.” amesema Mengi.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania, Godfrey Simbeye. 6 April, 2017.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania, Godfrey Simbeye. 6 April, 2017. Emmanuel Makundi/RFIKIswahili

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanznaia Godfrey Simbeye, amesema ukweli bado unabaki palepale kuwa licha ya hakikisho linalotolewa na Serikali kwa wawekezaji, bado mazingira ya uwekezaji kwa makampuni kutoka nje ni magumu.

Hata hivyo Simbeye amesema juma hili watakutana kwa mara nyingine na mawaziri kutoka wizara mbalimbali ambao wameagizwa na rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kukutana na sekta binafsi ili kuanisha changamoto zilizoko na kuangalia namna ya kuzimaliza.

Nao wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa wameeleza nia waliyonayo ya kuja kuwekeza nchini Tanzania, ambapo tayari baadhi ya makampuni yameshaanza mchakato wa awali kuanza kuwekeza nchini humo.

Hata hivyo na wao kwa nyakati tofauti wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuwepo kwa baadhi ya vikwazo ambavyo vinawafanya washindwe kuja kuwekeza kwa wakati mmoja lakini wakaeleza matumaini yao kuwa kwa hatua ambazo Serikali ya Tanzania imeanza kuchukua ni imani yao wataanza kuja kwa wingi nchini Tanzania.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.