Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA

Wataalamu: Usafiri bora wa uma na reli ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi

Wataalamu wa masuala ya miundombinu wanaoshiriki mkutano wa kwanza wa jukwaa la kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania, jijini Dar es Salaam, wameeleza kuridhishwa na mipango ambayo Serikali imeweka kuhusu kubadili na kuboresha baadhi ya miundo mbinu kwenye miji yake.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya safirishaji wakijadiliana wakati wa kongamano la kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania. April 5, 2017
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya safirishaji wakijadiliana wakati wa kongamano la kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania. April 5, 2017 Emmanuel Makundi/RFIKIswahili
Matangazo ya kibiashara

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa idhaa ya rfikiswahili, wataalamu hao wamesema baada ya siku tatu walizotumia kukaa jijini Dar es Salaam, wamegundua pamoja na changamoto za miundombinu zilizopo, wanaridhishwa na namna ambavyo idara za mipango miji zimeanza kuchukua hatua kutatua changamoto hizo.

Makamu wa rais wa kampuni ya SYSTRA Jean-Christophe Rouja inayojihusisha na ujenzi na ushauri kwa usafiri wa uma na reli, amesema binafsi amefurahishwa na namna ambavyo mradi wa mabasi yaendayo kasi maarufu nchini Tanzania kama BRT unavyofanya kazi na kuongeza kuwa hata nchi zilizoendelea zilishaanza kutumia usafiri wa aina hii toka kitambo na sasa umetatua shida ya usafiri wa uma kwenye miji mingi.

Rouja ameongeza kuwa “nimepata nafasi ya kutembelea stesheni ya treni ya Dar es Salaam na nimevutiwa kuona kuwa kuna mpango wa upanuzi wa kujenga reli ya kisasa ambayo naamini kwa kiasi kikubwa itatatua shida za usafiri wa kwenda mikoani kwa kutumia reli”.

Amesema kuwa kwa nchi kuendelea kiuchumi na hasa kwa kutumia usafiri wa reli ni lazima miundombinu yake ikarabatiwe na ijengwe kwenye kiwango kinachoridhisha.

Kwa upande wake mkurugenzi wa masuala ya masoko kutoka kampuni ya ALSTOM inayojihusisha na usafiri wa treni za kawaida na zile za umeme, Pierre Schwing, amesema kwa muda mfupi alioutumia nchini Tanzania, amegundua maeneo mengi ambayo wanaweza kutoa ushauri kwa Serikali na pengine kushirikiana katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya usafiri wa reli.

Schwing amesema licha ya iuwa jiji kama la Dar es Salaam linakadhia kubwa ya foleni, anaona bado Serikali inayo nafasi ya kushirikiana na makampuni makubwa ya reli kufanya upembuzi yakinifu kwenye miji yake mikubwa na kuangalia njia rahisi ambayo inaweza kutumika kubadili sura ya sekta ya usafirishaji nchini.

“Japo sijazunguka sana na hii ni mara yangu ya pili kuja Tanzania, nimeona kweli kuna maeneo ambayo inabidi Serikali iyafanyie kazi ili kuufanya usafiri wa uma uwe msaada kwa wananchi wake na kupunguza msongamano katikati ya jiji.” amesema Schwing.

Kwa upande wa sekta binafsi nchini Tanzania, wao wanaona kuwa bado Serikali haijawashirikisha vya kutosha hasa makampuni ya ndani yenye uwezo, hali ambayo inachangia kwa sehemu kubwa Tanzania kuonekana haina makampuni au wawekezaji wanaoweza kutengeneza miundombinu hii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.