Pata taarifa kuu
BURUNDI-MAUAJI-SIASA

Hisia mbalimbali zatolewa kufuatia mauaji ya Waziri wa Mazingira

Viongozi na watu mbalimbali nchini Burundi wameendelea kutoa hisia zao baada ya kuuawa siku ya Jumapili Januari 1, Waziri wa Maji, Mazingira na Mipango. Emmanuel Niyonkuru alipigwa risasi wakati alipokua akirudi nyumbani kwake, kwa mujibu wa polisi.

Wanajeshi wa Burundi katika mitaa ya mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, Mei 2015.
Wanajeshi wa Burundi katika mitaa ya mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, Mei 2015. REUTERS/Goran Tomasevic
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa serikali ametaja mauaji hayo kama "kitendo kiovu". Hata upande wa upinzani na mashirika ya kiraia wamelaani mauaji hayo.

Philippe Nzobonariba, msemaji wa serikali ya Burundi, ametaja mauaji hayo kama "kitendo kiovu" na amesema, katika taarifa yake kwamba, ni miongoni mwa mfululizo wa "mauaji ya kuvizia kwa viongozi waandamizi wa serikali", mauaji yanayoendeshwa na "magaidi", amesema Bw Nzobonariba .

Cnared, muungano wa upinzani unaoishi uhamishoni nje ya nchi pamona na vyama vya kiraia, wamelaani mauaji hayo. Akihojiwa na RFI, Gabriel Rufyiri, mwanzilishi wa shirika linalopambana dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa kiuchumi (OLUCOME) amesema kuwa analaani mauaji hayo na anataka wahalifu wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

"Leo hii kila mwananchi anaishi kwa hofu kwa sababu ya hali hii ya mauaji ya kuvizia. Viongozi kadhaa, watu wengi wasio na hatia waliuawa bila hata hivyo kufanyika uchunguzi ili wahalifu waadhibiwe kwa mujibu wa sheria, " Bw Rufyiri amesema.

"Hatutaki hotuba za kulaani. Hiyo haitoshi. Sisi, tunataka wananchi wa Burundi walindiwe usalama wao, na muhimu zaidi, kuwafikisha wahalifu hao wasioadhibiwa mbele ya vyombo vya sheria, "ameongeza Gabrie Rufyiri.

Dhana ya mauaji ya kisiasa

Kiongozi wa OLUCOME pia ameelezea masikitiko yake kuwa Waziri aliyeuawa hakuwa na ulinzi wa kutosha.

"Tunaamini kwamba mauaji haya ni ya kisiasa, " Gabriel Rufyiri amesema.

Itafahamika kwamba Emmanuel Niyonkuru ni waziri wa kwanza kuuawa toka kuibuka kwa machafuko nchini Burundi Aprili 2015.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.