Pata taarifa kuu
EU-TANZANIA

EU: Bunge la Tanzania kukataa mkataba wa EPA hakutaathiri ushirikiano wetu

Ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini Tanzania umesema kuwa, hautasitisha ushirikiano wowote na nchi ya Tanzania, licha ya bunge la nchi hiyo, kukataa kupitisha mkataba wa ushirikiano kati ya umoja huo na Tanzania, EPA.

Mkuu wa ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Balozi Roeland van de Geer, akiwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli
Mkuu wa ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Balozi Roeland van de Geer, akiwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli Ikulu/Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na wadau wa habari nchini Tanzania, mkuu wa ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini humo, Roeland van de Geer, amesema kuwa, mkataba wa ushirikiano, EPA, hauna uhusiano wowote na ushirikiano ambao upo kati ya Tanzania na umoja huo.

Balozi, Roeland van de Geer, alikuwa akijibu swali na mmoja wa wadau wa habari aliyetaka kufahamu ikiwa Jumuiya ya Ulaya itachukua hatua zozote kwa nchi ya Tanzania baada ya bunge kukataa Serikali kutia saini mkataba huo.

Akizungumza na mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya RFI, balozi De Geer amesema kuwa "hapana! hatutasitisha makubaliano yetu mengine ya kibishara na Tanzania, wala kusitisha misaada yetu kwa Tanzania, eti kwa sababu wabunge walikataa Serikali kutia saini mkataba huu".

Mkuu huyo wa ujumbe wa Ulaya nchini Tanzania ameongeza kuwa, Tanzania ni nchi huru na hakuna anayeweza kuiamulia cha kufanya ikiwa haikufurahishwa na mkataba huu wala mkataba mwingine wowote.

De Geer amesema kuwa, kwa sasa umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye maeneo mengine, wakati mazungumzo yakiendelea kuhusu uwezekano wa kutiwa saini kwa makubaliano haya ya ushirikiano katika siku zijazo.

De Geer amesema kuwa, sera ya umoja wa Ulaya ni mazungumzo na ndio maana mara zote wakati wa majadiliano haya yaliyochukua takribani miaka 10, mara zote wamekuwa wakiheshimu mitazamo na misimamo ya nchi ambazo zinataka kutia saini mkataba huu.

Mkataba wa EPA ni suala ambalo hata wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatofautiana pakubwa, kwa kuwa hata kwenye mkutano wao wa mwisho uliofanyika jijini Dar es Salaam, walishindwa kukubaliana na kujipa muda zaidi.

Hii ina maana kuwa nchi pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ambayo imekubali mkataba huu ni nchi ya Kenya, ambayo tayari imekubali kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa bado una imani kuwa siku moja ndoto ya kutiwa saini kwa mkataba huu itatimia, na kwamba utaendelea kutoa msaada wa aina yoyote kwa Tanzania kuhusu kufahamishana zaidi faida na hasara za mkataba wenywe katika siku za usoni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.