Pata taarifa kuu
KENYA

Mke wa Aboud Rogo afikishwa Mahakamani mjini Mombasa

Haniya Said Saggar, mke wa aliyekuwa Mhubiri wa Kiislamu Aboud Rogo aliyeuawa mwaka 2012 baada ya kushukiwa kutoa mafunzo ya itikadi kali na kuliunga mkono kundi la Al Shabab mjini Mombasa, amefikishwa Mahakamani mjini Mombasa nchini Kenya kujibu mashtaka ya ugaidi.

Haniya Said Saggar, mke wa aliyekuwa mhubiri wa Kiislamu Sheikh Aboud Rogo akiwa Mahakamani mjini Mombasa Septemba 15 2016
Haniya Said Saggar, mke wa aliyekuwa mhubiri wa Kiislamu Sheikh Aboud Rogo akiwa Mahakamani mjini Mombasa Septemba 15 2016 www.nation.co.ke
Matangazo ya kibiashara

Saggar alikamatwa siku ya Jumatano na maafisa wa polisi kwa madai ya kushirikiana na wanawake watatu waliouawa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuvamia kituo cha polisi mjini Mombasa.

Kukamatwa kwake kunafikisha idadi ya wanawake waliokamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi kufikia wanne.

Wanawake hao raia wa Somalia wanazuiliwa wakati huu polisi wakiendelea na uchunguzi dhidi yao akiwemo Saggar.

Kizazaa kilizuka Mahakamani baada ya mtoto wa Saggar, Dhulkifli Rogo kuvunja Kamera ya Mwanahabari wa Shirika la Habari la Reuters aliyekuwa anampiga picha mama yake.

Polisi nchini Kenya wanasema kuwa, kundi la Al Shabab ambalo kwa sasa linashirikiana na Islamic State limeanza kutumia wanawake kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Aidha, ripoti za maafisa wa usalama zinasema kuwa wanawake na wanaume zaidi ya 100 walikwenda nchini Syria na Iraq kupata mafunzo ya kigaidi kutoka kwa wapiganaji wa Islamic State.

Kenya inaendelea kukabiliana na ugaidi tangu mwaka 2012, ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia kukabiliana na wanamgambo wa Al Shabab.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.