Pata taarifa kuu
OLIMPIKI-BRAZIL 2016-RIADHA

Vivian Cheruiyot aishindia Kenya medali ya kwanza ya dhahabu mbio za Mita 5000

Vivian Cheruiyot, ameishindia Kenya medali ya kwanza ya dhahabu katika mbio za Mita 5000 kwa upande wa wanawake katika Michezo ya Olimpiki inayomalizika siku ya Jumapili nchini Brazil.

Vivian Cheruiyot akisherehekea baada ya kuishindia Kenya medali ya dhahabu katika mbio za Mita 5000 katika Michezo ya Olimpiki nchini Brazil Agosti 20 2016
Vivian Cheruiyot akisherehekea baada ya kuishindia Kenya medali ya dhahabu katika mbio za Mita 5000 katika Michezo ya Olimpiki nchini Brazil Agosti 20 2016 Olympic games 2016
Matangazo ya kibiashara

Cheruiyot, ambaye alimaliza wa pili na kushinda medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 jijini London nchini Uingereza katika mbio hizi, aliweka rekodi mpya ya Olimpiki baada ya kumaliza kwa muda wa dakika 14 sekunde 26 nukta 18.

Nafasi ya pili ilimwendea Mkenya mwingine, Hellen Obiri aliyemaliza kwa muda wa dakika 14 sekunde 29 nukta 77 na kuishindia nchi yake medali ya fedha.

Almaz Ayana raia wa Ethiopia, aliyeshinda medali ya dhahabu katika mbio za Mita 10000 katika Michezo hii wiki iliyopita, alimaliza katika nafasi ya tatu na kuishindia nchi yake medali ya shaba.

Vivian Cheruiyot baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mbio za Mita 5000 kwa upande wa wanawake Agosti 20 2016 nchini Brazil katika Michezo ya OLimpiki
Vivian Cheruiyot baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mbio za Mita 5000 kwa upande wa wanawake Agosti 20 2016 nchini Brazil katika Michezo ya OLimpiki olympic.org

Cheruiyot mwenye umri wa miaka 32 aliyemaliza wa pili katika mbio za Mita 10000 katika Michezo hii, amesema amefurahi sana kushinda medali ya dhahabu kwa sababu; amekuwa akishiriki Michezo ya Olimpiki bila ya kupata dhahabu.

Mwanariadha huyu anayeingia katika vitabu vya historia kwa kuishindia Kenya medali ya kwanza katika mbio za Mita 5000 kwa upande wa wanawake, baada ya kuanza kutafuta medali ya dhahabu tangu alipoanza kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2012.

Hellen Obiri (Kushooto) akiwa amejivuka bendera ya taifa la Kenya baada ya Vivian Cheruiyot (Kulia) kushinda medali ya dhahabu mbio za Mita 5000 Michezo ya Olimpiki Brazil Agosti 20 2016
Hellen Obiri (Kushooto) akiwa amejivuka bendera ya taifa la Kenya baada ya Vivian Cheruiyot (Kulia) kushinda medali ya dhahabu mbio za Mita 5000 Michezo ya Olimpiki Brazil Agosti 20 2016 olympic.org

Kenya sasa inashikilia nafasi ya 16 duniani na ni ya kwanza barani Afrika kwa medali 10 zikiwemo tano za dhahabu na zingine tano za fedha.

Marekani inaongoza kwa wingi wa medali, baada ya kujizolea 105, zikiwemo 38 za dhahabu.

Uingereza ni ya pili kwa medali 60, 24 za dhahabu huku China ikiwa ya tatu kwa medali 65.

Nafasi ya nne inashikiliwa na Ujerumani ambayo ina medali 35 huku Urusi ikimaliza tano bora kwa medali 48.

Siku ya Jumamosi kutakuwa na fainali ya mbio za Mita 800 kwa upande wa wanawake, fainali ya mbio za Mita 1500 kwa wanaume na 5000 kwa wanaume.

Michezo hii itahitimishwa siku ya Jumapili kwa mbio za Marathon kwa upande wa wanaume, mbio ambazo zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutoka kwa wanariadha kutoka nchi za Afrika Mashariki Kenya, Uganda na Ethiopia.

Bingwa mtetezi wa mbio hizi ni Mganda Stephen Kiprotich, aliyeshinda katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2012 jijini London.

Michezo ijayo ya Olimpiki itafanyika jijini Tokyo Japan mwaka 2020.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.