Pata taarifa kuu
KENYA-Siasa

Rais wa kenya akataa katu katu kukutana kwa mazungumzo na upinzani

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufika tarehe 7 ya mwezi julai, siku ambayo muungano wa upinzani nchini Kenya CORD umetangaza kuitisha maandamano ya nchi nzima iwapo Serikali haitafanya mazungumzo nao, rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameendelea kusisitiza msimamo wake kuhusu kutokubali mazungumzo haya.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akikataa kukutana kwa mazungumzo na muungano wa CORD.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akikataa kukutana kwa mazungumzo na muungano wa CORD. Reuters/Noor Khamis
Matangazo ya kibiashara

Rais Kenyatta amewataka wanasiasa na wananchi wa Kenya kuachana na siasa za majitaka na ukabila na badala yake kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki shughuli za maendeleo katika harakati za kulijenga taifa la Kenya.

Kauli ya rais Kenyatta kusisitiza wanasiasa kuachana na siasa mbaya na za kikabila anaitoa wakati huu muungano wa upinzani ukiendelea na mikutano yake kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 7 ya mwezi ujao kushinikiza serikali kuwa na mazungumzo ya kitaifa.

Wakati hayo yakijiri waziri wa usalama nchini Kenya, Josephu Ole Lenku ameendelea kuushambulia muungano wa upinzani nchini Kenya CORD akidai kuwa wanasiasa wake ndio wamekuwa vinara wa kuchochea kuharibika kwa usalama nchini humo.

Waziri Ole Lenku anasema kuwa wana ushahidi na uhakika wa kutosha kuwa wanasiasa wa muungano wa CORD wamekuwa wakisajili vijana wa kundi la Mungiki pamona na Al-shabab kwa lengo la kuzorotesha usalama nchini humo na kuifanya nchi kutotawalika.

Matamshi ya Ole Lenku anayatoa wakati huu baadhi ya wabunge wa muungano huo wakiwa wamewasilisha muswada maalumu Bungeni kuwataka wabunge kumfuta kazi kiongozi huyo.

Hata hivyo waziri Ole Lenku ameendelea kutetea uamuzi wake na kuwaonya wanasiasa wanaoendeleza maneno ya chuki na kusajili vijana kwenye makundi haramu nchini humo.

Hata hivyo kinara mwingine wa CORD, Moses Wetangula ametupilia mbali madai ya Ole Lenku akimtaka kuwasilisha ushahidi wake polisi ama kuwakamata viongozi wote wanaohusishwa na makundi hayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.