Pata taarifa kuu

Miaka 30 baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, waathiriwa wa ubakaji wanaanza kupata amani

Mbali na vifo 800,000, wasichana na wanawake wapatao 250,000 walibakwa na Wahutu wenye msimamo mkali wakati wa mauaji ya kimbari. Kwao na kwa watoto 20,000 waliozaliwa kutokana na ubakaji huu, makovu ya mauaji ya kimbari yamekuwa magumu kupona.

Nguo za wahanga zilizogunduliwa wkatika kaburi la pamoja baada ya mauaji ya kimbari.
Nguo za wahanga zilizogunduliwa wkatika kaburi la pamoja baada ya mauaji ya kimbari. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Kila mwaka, mwezi wa Aprili unapofika na ukumbusho wa mauaji ya halaiki ya Watutsi yanapofika, Agatha* anazima redio na kujizungusha kwa ukimya, akitumia muda wake mwingi akiwa amejilaza kitandani mwake. Siku moja mwaka wa 2006, binti yake Agnès * alimwomba nyanya yake amweleze. Majibu yalimwacha msichana huyo, aliyekuwa na umri wa miaka kumi hivi, katika mshtuko.

“Nililia na mara moja nikaanza kumuogopa mama yangu kwa sababu nilihisi kama nilikuwa jeraha katika nafsi yake,” anasema Agnès, ambaye sasa ana umri wa miaka 28.

Mama yake, pamoja na nyanyake, walikuwa miongoni mwa takriban wasichana na wanawake 250,000 waliobakwa na Wahutu wenye msimamo mkali wakati wa mauaji ya halaiki ambayo yalilenga Watutsi walio wachache nchini Rwanda kati ya mwezi Aprili na Julai 1994, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa. Takriban watu 800,000, hasa Watutsi lakini pia Wahutu wenye msimamo wa wastani, waliuawa katika kipindi cha miezi mitatu ya mauaji hayo.

Alibakwa na kutekwa nyara na aliyekuwa mwanafunzi wa Kihutu kutoka shuleni kwake, Agatha alimzaa Agnès akiwa na umri wa miaka 17, katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania ambako mtekaji wake alimbeba, akikimbia kisasi baada ya kuanguka kwa utawala wa kimbari uliopinduliwa na waasi wa Kitutsi wa Rwandan Patriotic Front (RPF), mwishoe mtekaji nyara huyo alifariki muda mfupi baadaye.

Ndugu za Agatha walimsihi amuue mtoto. Alikataa. Hata hivyo, kila alipomtazama Agnes, aliona maisha yake ya baadaye yakiwa yameharibika, ndoto yake ya kuwa daktari wa mifugo na kutunza mifugo ya familia ilitoweka.

Ubaguzi dhidi ya Watutsi ulikuwa wa mara kwa mara kabla ya mauaji ya kimbari, ikiwa ni pamoja na shuleni ambapo walimu wa Kihutu hawakuficha dharau yao kwa wanafunzi wa Kitutsi. Lakini hakuwaza kamwe kuona baba yake akiuawa mbele ya macho yake na mwili wake kutupwa kwenye choo na jirani yake kutoka kabila la Wahutu.

Aliporejea katika wilaya ya Ngoma mashariki mwa Rwanda mwaka 1996, kila kitu kilikuwa kimebadilika. Hakuna tena ng'ombe, pesa kidogo na Agatha alikuwa "mtoto aliyezaa mtoto", kama anavyojielezea. “Ni Mungu aliyemlea, si mimi. Sikuwa na uwezo wowote,” anaeleza mwanamke huyo, ambaye sasa ana umri wa miaka 45 na mama wa watoto saba.

Agnès alikataliwa na familia yake yote. Kwa upande wa baba yake Mhutu, aliitwa "nyoka", akirejea maneno ya chuki dhidi ya Watutsi ambayo yalichochea mauaji hayo. Familia yake ya Kitutsi ya upande wa mama yake ilibaini kwamba damu ya wahusika wa mauaji ya kimbari ilitiririka kupitia mishipa yake.

Alijihisi kama mgeni katika familia yake mwenyewe, aliondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka 16, na kujipatia riziki akiwa mhudumu au kahaba. Anarudi kijijini kwao miaka saba baadaye, baada ya mume wake wa kwanza kumwacha alipogundua kwamba Agnès "alizaliwa kwa ubakaji".

Aliolewa tena na kupata mtoto wa pili. Kwa miaka mitano iliyofuata, Agnès na Agatha waliishi katika maisha magumu, wakipuuza maisha yao mabaya ya zamani.

"Njia ndefu"

Ingawa serikali ya Rwanda iliunda mahakama za kijamii (Agacaca) mwaka 2002 kuruhusu waathiriwa kusikiliza "ungamo" la wauaji, mateso ya walionusurika ubakaji na watoto wao hayakuzingatiwa. Watoto waliozaliwa kutokana na ubakaji - karibu 20,000, kulingana na Shirika lisilo la Kiserikali la Survivors Fund - hawatambuliwi kama waathirika wa mauaji ya kimbari na serikali.

Mnamo 2020, sehemu ya Rwanda ya shirika lisilo la kiserikali la Interpeace liliandaa warsha kushughulikia kiwewe hiki cha kizazi kiitwacho "Mvura Nkuvure" ("Niponye, ​​nikuponya", kwa Kinyarwanda). Mwaka jana, Agatha alishiriki katika mojawapo ya warsha hizi. Kwa miezi mitatu, hakusema neno. Alisikiliza hadithi za washiriki wengine na kulia.

Agnès alikuwa sehemu ya kikundi kingine. Siku moja mnamo mwezi Agosti, alizungumza na maneno yakamwagika: "Mara moja nilihisi utulivu, moyo wangu ulikuwa mwepesi kwa sababu nilikuwa nimesema mambo ambayo nilikuwa naogopa kusema kila wakati." Aibu ilitoweka na pamoja nayo, hasira yake kwa mama yake. "Niligundua kwamba kile ambacho hakunipa, hakuwa nacho," anaeleza.

Ana matumaini kidogo ya kuanzisha tena uhusiano na familia yake kubwa, ingawa anasema amewasamehe. Kwa Clenie, mwezeshaji aliyesimamia warsha, "bado kuna safari ndefu ya kuiponya Rwanda, lakini tumepiga hatua."

Huku kumbukumbu za maadhimisho ya miaka 30 ya mauaji ya halaiki zikikaribia, Agatha anasema anahisi kuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali tangu mwaka 1994. "Kuna picha ambazo huwezi kuzifuta, hata ujaribu kwa bidii kiasi gani. Lakini nina ujasiri wa kutosha kukabiliana na kumbukumbu mbaya zinapotokea,” amesema. “Sihisi huzuni tena ninapomtazama Agnès,” anaongeza hivi: “Ninahisi kupendwa tu.”

*Majina ya kwanza yamebadilishwa

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.