Pata taarifa kuu
NJAA-USALAMA

Watoto milioni 1.6 nchini Sudan Kusini wako hatarini kwa utapiamlo mwaka 2024

Zaidi ya watoto milioni 1.6 walio chini ya umri wa miaka mitano wako hatarini kukumbwa na utapiamlo mwaka 2024 nchini Sudan Kusini kutokana hasa na matokeo ya mafuriko, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limeonya siku ya Jumatatu.

Watu waliohamishwa makazi yao wakichuna majani kwenye matawi, wakijiandaa kuyachemsha na kuyala katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini, Mei 5, 2023.
Watu waliohamishwa makazi yao wakichuna majani kwenye matawi, wakijiandaa kuyachemsha na kuyala katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini, Mei 5, 2023. Β© AP
Matangazo ya kibiashara

Nchi changa zaidi duniani, Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na machafuko ya kudumu na ghasia za kisiasa za kikabila tangu uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011.

Nchi hii yenye wakazi wapatao milioni 11 pia inakabiliwa na hali mbaya ya hewa, ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa yenye athari zinazoweza kuangamiza mamilioni ya watu.

"Tunaona ongezeko la kutisha sana la utapiamlo" kutokana na mafuriko na msongamano wa watu unaoripotiwa katika baadhi ya maeneo, amesisitiza katika taarifa mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini, Mary-Ellen McGroarty, akiongeza: "Watoto wadogo ndio wanaoteseka zaidi.

"Zaidi ya watoto milioni 1.6 walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mwaka 2024," taarifa hiyo imeongeza.

Mnamo mwezi Mei, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) ​​​​lilibainisha kwamba utapiamlo ulitishia watoto milioni 1.4 mnamo mwaka 2023.

Taarifa hasa inataja hali katika kaunti ya Rubkona (kaskazini), ambapo maji yamezamisha maeneo makubwa ya ardhi, na kulazimisha jamii nzima kuishi kwenye visiwa vidogo tangu mwaka 2021. Gharama ya vyakula vya msingi katika eneo hilo imepanda kwa zaidi ya 120% tangu mwezi Aprili.

"Huu ndio ukweli wa maisha katika mstari wa mbele wa shida ya hali ya hewa," anasema Mary-Ellen McGroarty.

Mgogoro huo umezidishwa na wimbi la mamia kwa maelfu ya Wasudan Kusini wanaokimbia vita nchini Sudan, ambao wanajikuta katika hali ya "dharura ya chakula".

Vita kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdane Daglo ambavyo vilianza Aprili 15, vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 9,000, kulingana na makadirio ya shirika lisilo la kiserikali la Armed Conflict Location & Event Data Project (Acled), ambayo yanachukuliwa kuwa yanaweza kuwa juu zaidi.

Sudan Kusini, mojawapo ya nchi zenye maendeleo duni zaidi duniani licha ya rasilimali zake za mafuta, ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2013 na 2018, ambavyo vilisababisha vifo vya karibu watu 400,000 na mamilioni kuyahama makazi yao.

Umoja wa Mataifa mara kwa mara umewanyooshea kidole cha lawama viongozi wa Sudan Kusini kwa wajibu wao wa ghasia, ukandamizaji wa uhuru wa kisiasa na ufisadi.

Sudan Kusini inakabiliwa na "mgogoro mkubwa wa kibinadamu," kulingana na Benki ya Dunia, ambayo ilikadiria mnamo mwezi Septemba kwamba karibu watu milioni 9.4, au 76% ya watu, walihitaji msaada wa kibinadamu mnamo mwaka 2023.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.