Bernard Membe, Waziri wa zamani wa Mambo ya nje wa Tanzania afariki dunia
NAIROBI – Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe amefariki dunia, jijini Dar es salaam.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Rais Samia Suluhu Hassan, amesema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Membe, ambaye pia aliwahi kuwania urais mwaka 2020, kupitia chama cha ACT Wazalendo.
“Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi,” ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi. Pole kwa familia, ndugu, jamaa & marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina. pic.twitter.com/tqN34ubqtC
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) May 12, 2023
Ripoti kutoka kwa aliyekuwa Msaidizi wake, Allan Kiluvya zimesema, Membe aliugua kwa muda mfupi na kukimbizwa hospitalini, Ijumaa Alfajiri na baadaye akafariki.
Alihudumu katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 2007 hadi 2015, wakati wa uongozi wa rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Membe aliwahi pia kuwa Mbunge wa jimbo la Mtama, alikochaguliwa mwaka 2000 na kuhudumu hadi mwaka 2015.
Shirika la habari linalomilikiwa na serikali nchini humo pia limethibitisha kifo cha Membe.
Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, amefariki dunia muda mfupi uliopita katika hospitali ya Kairuki mkoani Dar es Salaam.
— TBCOnline (@TBConlineTZ) May 12, 2023
Taarifa za awali zinaeleza kuwa Membe alipata changamoto ya kifua na kupelekwa alfajiri ya leo hospitalini hapo na baadaye kufariki dunia. pic.twitter.com/FBHAWofPEt