Pata taarifa kuu

Rais Tshisekedi wa DRC ameshutumu utendakazi wa wanajeshi wa Afrika Mashariki

NAIROBI – Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amelishtumu jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutofanya vya kutosha kudhibiti utovu wa usalama Mashariki mwa nchi yake.

Rais Félix Tshisekedi wa DRC amekosoa utendakazi wa kikosi cha Afrika Mashariki nchini mwake
Rais Félix Tshisekedi wa DRC amekosoa utendakazi wa kikosi cha Afrika Mashariki nchini mwake AFP - JACQUES WITT
Matangazo ya kibiashara

Tshisekedi ametoa kauli hiyo katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Botswana na kudai kuwa kikosi hicho kinashirikiana na waasi wa M 23 na huenda kikaondoka nchini mwake kufikia mwisho wa mwezi Juni.

Kazi ambayo kikosi hiki kilipewa haijatekelezwa kabisa, leo tumeona katika baadhi ya maeneo ushirikiano kati ya kikosi cha jumuiya na waasi wa M23 kinyume na ilivyopangwa kwenye makubaliano. alisema rais Felix Tshisekedi

00:32

Rais wa DRC Felix Tshisekedi amekosoa utendakazi wa kikosi cha EAC mashariki mwa nchi yake

Kauli yake inakuja siku moja baada ya mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya SADC nchini Namibia, ambako jumuiya hiyo imesema itatuma vikosi vyake Mashariki mwa DRC.

Matamshi yake pia yanakuja baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kamanda wa kikosi hicho nchini DRC Jenerali Jeff Nyagah katika kile kilichodaiwa ni kutokuwepo kwa maelewano na uongozi wa nchi hiyo ambao pia ulikosoa utendakazi wake.

Meja generali Jeff Nyagah, aliyekuwa mkuu wa vikosi vya EACRF nchini DRC
Meja generali Jeff Nyagah, aliyekuwa mkuu wa vikosi vya EACRF nchini DRC © EACRF

Aidha mkuu huyo wa DRC alisema kuwa muda wa vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki utakapofika tamati mwishoni mwa mwezi Juni watafanya tathmini kuona iwapo kikosi hicho kitakuwa kimefanya kazi yake na baadae watafanya maamuzi kuona namna watakavyolinda nchi yao ya Kongo.

Wanajeshi wa EAC wanaopambana na makundi ya waasi mashariki ya DRC
Wanajeshi wa EAC wanaopambana na makundi ya waasi mashariki ya DRC AP - Ben Curtis

Kando na rais Tshisekedi kukosoa jukumu na uwezo wa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, raia nchini humo pia nao wamekuwa na kauli sawa na kiongozi wakituhumu wanajeshi hao kwa kukosa kutekeleza walivyotarajiwa kufanya.

Licha ya uwepo wa vikosi hivyo katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na makundi yenye silaha ikiwemo M23, mashambulio dhidi ya raia yamekuwa yakiendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo ya mashariki ya DRC.

Waasi wa M23 wanatuhumiwa kwa kuhangaisha usalama wa raia mashariki mwa DRC
Waasi wa M23 wanatuhumiwa kwa kuhangaisha usalama wa raia mashariki mwa DRC AP - Moses Sawasawa

Japokuwa wanajeshi hao wanatuhumiwa kwa kukosa kuwakabili waasi, baadhi ya raia wameeleza kuwa wamerejea katika makazi yao ya zamani baada ya M23 kuondoka na kupeana sehemu kwa jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nchi za SADC zinajumuisha Afrika Kusini, Angola, Tanzania, Namibia, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe na DRC.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.