Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakutana kujadili usalama Mashariki mwa DRC
Marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekutana jijini Bujumbura nchini Burundi katika mkutano usiokuwa wa kawaida, kujadiliana kuhusu kuendelea kwa mzozo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Imechapishwa:
Viongozi hao wamekutana kutathmini mwenendo wa hali ya usalama, Mashariki mwa DRC na nini cha kufanya kurejesha amani, katika kipindi hiki ambacho waasi wa M23 wanapoendelea kupambana na vikosi vya DRC na kuchukua maeneo zaidi.
Rais wa DRC Felix Thisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, ambao nchi zao hazina uhusiano mzuri wa kidiploamsia kuhusu madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23 pia wamehudhuria.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Yoweri Museveni wa Uganda, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, William Ruto wa Kenya na mwakilishi wa Sudan Kusini.
Mkutano huu umekuja siku chache baada ya Rwanda kukiri kushambulia ndege ya kivita ya DRC, baada ya kudai kuwa ilivuka mpaka na kuingia kwenye angaa lake kinyume cha sheria.
DRC nayo imewafukuza wanajeshi wa Rwanda, waliokuwa katika ujumbe wa jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hizi ni baadhi ya changamoto zinazosubiri viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuyatafutia ufumbuzi.