Pata taarifa kuu
KENYA-KAMPENI- UCHAGUZI-2022

Kenya 2022: Kampeni zamalizika kuelekea Uchaguzi wa Agosti 9

Kampeni nchini Kenya, zimemalizika siku ya Jumamosi, kuelekea uchaguzi mkuu Jumanne ijayo.

Picha za wagombea urais nchini Kenya, Raila Odinga (Kushoto), William Ruto (Kulia) katika kipindi cha kampeni
Picha za wagombea urais nchini Kenya, Raila Odinga (Kushoto), William Ruto (Kulia) katika kipindi cha kampeni AFP - SIMON MAINA
Matangazo ya kibiashara

Wagombea wakuu wanaowania urais, naibu rais William Ruto mwenye umri wa miaka 55,  na Raila Odinga mwenye umri wa miaka 77, wamemalizia kampeni zao jijini Nairobi na kuwaomba kwa mara ya mwisho wananchi kuwapigia kura na kuahidi mabadiliko iwapo wataingia madarakani.

Wafuasi wa mgombea urais, Raila Odinga, waliojitokeza kuhudhuria mkutano wa mwisho wa kampeni, katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Agosti, 06, 2022
Wafuasi wa mgombea urais, Raila Odinga, waliojitokeza kuhudhuria mkutano wa mwisho wa kampeni, katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Agosti, 06, 2022 © FMM-RFI

Odinga, ambaye aliwahi kuhudumu kama Waziri Mkuu,amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura ili kupata ushindi mapema.

"Tupige kura mapema, tushinde mapema," amesema Odinga.

Aidha, ameeleza kuwa atakuwa tayari kusalimia na mpinzani wake (William Ruto) iwapo atashinda au kushindwa uchaguzi huu.

"Nitakuwa tayari kusalimia na wapinzani wangu, baada ya uchaguzi kwa sababu, naipenda Kenya kuliko Raila Odinga," amesema.

Adimo Evance, mfuasi wa Odinga, aliyehudhuria mkutano wa mwisho wa Odinga katika uwanja wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi, amesema atampigia Odinga kwa sababu ya ahadi yake ya kupambana na ufisadi.

"Nitampigia Odinga kwa sababu, ameapa kupambana na ufisadi, lakini pia ni mpenda amani," amesema.

Mfuasi wa Raila Odinga, aliyehudhuria mkutano wa siasa, Agosti, 06 2022
Mfuasi wa Raila Odinga, aliyehudhuria mkutano wa siasa, Agosti, 06 2022 © FMM-RFI

Ruto naye amewataka wapinzani wake kujitokeza kwa wingi na kumchagua kuwa rais, huku naye akisema atakuwa tayari kukutana na wapinzani wake baada ya uchaguzi.

Naibu huyo wa rais pia amewataka Wakenya kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura.

"Mjitokeze kwa wingi, tupige kura asubuhi," amesema.

Wafuasi wa William Ruto wakiwa katika uwanja wa Nyayo, Jumamozi Agosti, 06 2022
Wafuasi wa William Ruto wakiwa katika uwanja wa Nyayo, Jumamozi Agosti, 06 2022 © FMM-RFI

Aidha,amesema atakuwa tayari kukutana na kunywa chai na mpinzani wake Raila Odinga, baada ya uchaguzi.

" Nitakuwa tayari kunywa chai na mpinzani wangu, sio vinginevyo," amesema Ruto.

Janet Munyesi mfuasi wa Ruto, aliyejokeza kwenye mkutano wake wa mwisho kwenye uwanja wa Nyayo, amesema atampigia kura kwa sababu ya ahadi ya kupambana na umasikini.

" Nampenda Ruto kwa sababu anawatetea masikini, " amesema Munyesi.

Mfuasi wa William Ruto, aliyewasili mapema kuhudhuria mkutano wa mwisho wa kampeni, uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Agosti 06 2022
Mfuasi wa William Ruto, aliyewasili mapema kuhudhuria mkutano wa mwisho wa kampeni, uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Agosti 06 2022 © FMM-RFI

Wagombea wengine wanaowania urais ni pamoja na Profesa George Wajackoyah wa chama cha Roots na David Mwaure kutoka chama cha Agano.

Mambo muhimu kuhusu uchaguzi huu

Tume ya Uchaguzi iliwasajili wapiga kura Milioni 22.1.

Karu asilimia 40 ya wapiga kura , karibu Milioni 8.8 ni kati ya umri kati ya miaka 18 hadi 34.

Kuna vituo 46,229 vya kupigia kura na, vitafunguliwa kati ya saa 12 asubuhi na kufungwa saa 11 jioni.

Kuna wagombea, 16,100 wanaowania nyadhifa mbalimbali.

Kutangazwa kwa matokeo

Tume ya Uchaguzi, ina siku saba, kutangaza matokeo ya mwisho ya urais.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa Agosti 16, jijini Nairobi.

Iwapo hakutakuwa na mshindi katika mzunguko wa kwanza kwa kupata asilimia 50 ya kura zote na asilimia nyingine 25 katika nusu ya Kaunti 47, kutakuwa na mzunguko wa pili baada ya siku 30.

Iwapo, hakutakuwa na mgombea atakayewakilisha kesi katika Mahakama ya Juu, kupinga atakayekuwa ametangazwa mshindi, ataapishwa na kuwa rais baada ya wiki mbili.

Lakini iwapo, Mahakama itafuta matokeo, uchaguzi mwingine utafanyika baada ya siku 60.

Mwaka 2017 ushindi wa rais Uhuru Kenyatta, ulifutwa na Mahakama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.