Pata taarifa kuu
KENYA-RUTO-SIASA

Siasa nchini Kenya: Safari ya kisiasa ya mgombea urais William Ruto

Naibu rais William Ruto anawania urais kwa mara ya kwanza, ahadi yake kuu ikiwa ni kuimarisha maisha ya Wakenya wa chini kupitia sera yake ya kiuchumi anayouita Bottom up.

William Ruto, naibu rais wa Kenya
William Ruto, naibu rais wa Kenya REUTERS - BAZ RATNER
Matangazo ya kibiashara

Ruto mwenye umri wa miaka 55, aliwahi pia kuwa mbunge wa jimbo la Eldoret Kaskazini, lakini pia Waziri wa Kilimo na Elimu ya Juu wakati wa serikali ya muungano kati ya mwaka 2007-2013.

Alianza siasa, mapema miaka ya tisini katika vuguvugu la vijana katika chama tawala wakati huo KANU lililofahamika kwa jina la YK92, wakati wa uongozi wa rais wa zamani Hayati Daniel arap Moi.

Ruto ambaye anajiita Hustler, ikiwa na maana ya mtu aliyetokea katika maisha ya chini ya kupanda hadi kuwa tajiri, aliwahi kuwa mwandani wa kisiasa wa mpinzani wake wa sasa Raila Odinga, wakati huo wakiwa katika chama cha ODM.

Baada ya vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007, Ruto alikuwa miongoni mwa watu sita, walioshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC na kushtakiwa kwa kupanga na kuchochea vurugu hizo, zilizosababisha zaidi ya watu Elfu moja kupoteza maisha, lakini kesi hiyo ikafutwa baada ya ukosefu wa ushahidi.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2013 alijiunga na Uhuru Kenyatta na kuwa mgombea mwenza wake na kushinda uchaguzi huo, lakini pia mwaka 2017.

Hata hivyo, mwaka 2018 wakati rais Kenyatta aliposalimia na kiongozi wa upinzani Raila Odinga maarufu kama Handshake, alianza kutofautiana na Kenyatta na uhusiano wao wa kisiasa ukawa mbaya mpaka kipindi hiki cha uchaguzi.

Wanaompenda Ruto wanasema ni kiongozi shupavu, lakini wakosoaji wake wanamweleze kama mwanasiasa mwenye tamaa ya mali hasa ardhi huku wengine wakimtuhumu kuwa mfisadi, madai anayosema yanalenga kumchafua kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.