Pata taarifa kuu
KENYA-ICC-Sheria-Haki za binadamu

Rais Kenyatta arejea nchini na kupokelewa kwa kishindo

Hatimaye rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amewasili muda mfupi uliopita nchini mwake akitokea mjini The Hague Uholanzi ambapo hapo jana alihudhuria kikao cha kuamua hatma ya kesi yake kwenye Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC ambapo anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu.  

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta asikilizwa na majaji wa ICC mjini Hague, Oktoba 8 mwaka 2014.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta asikilizwa na majaji wa ICC mjini Hague, Oktoba 8 mwaka 2014. REUTERS/Peter Dejong
Matangazo ya kibiashara

Rais Kenyatta amepokelewa na naibu wake, William Ruto pamoja na viogozi wengine wa Serikali, ambapo kumefanyika shughuli za kukabidhiana madaraka yeye na naibu wake ambaye kwa siku mbili alikuwa akikaimu nafasi yake.

Hapo jana rais Uhuru Kenyatta amehudhuria kikao maalum kuhusu kesi inayomkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC mjini Hague nchini Uholanzi.

Rais Kenyatta aliwasili katika Mahakama hiyo jumatano wiki hii, akionekana mchangamfu huku akipokelewa nje ya Mahakama hiyo na baadhi ya wabunge na wafuasi wake waliofika mjini Hague.

Kilichofanyika katika kikao hicho ni upande wa mashtaka kuomba Majaji kuahirisha kesi hiyo kwa muda usiojulikana ili kukusanya ushahidi wa kutosha , huku upande wa utetezi ukitaka kesi hiyo kusitishwa.

Kiongozi wa Mashtaka Fatoue Bensuda amekanusha tuhma za Mawakili wa Kenyatta kuwa, Ofisi yake imekosa ushahidi kuendeleza kesi hiyo na kuwaambia majaji kuwa kinachokosena tu ni ushahidi wa kutosha.

Kwa upande wake wakili wa rais Kenyatta Steven Kay, amewaambia Majaji hao kuwa wakati umefika kwa kesi hiyo kusitishwa, na rais Kenyatta kuwa huru dhidi ya tuhma za kuchochea na kufadhili machafuko ya baada ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Baada ya kuondoka Mahakamani, rais Kenyatta akizungumza na wakenya nje ya Mahakama hiyo amesema ana matumaini kuwa kesi hiyo itasitishwa.

Kinachosalia sasa ni Majaji wa Mahakama hiyo wakiongozwa na Kuniko Ozaki kuamua ikiwa kesi hiyo itaahirishwa kwa muda usiojulikana au itasitishwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.